Na Nasra Bakari, TimesMajira Online
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi, ameitaka ofisi yake kujikita katika utafiti wa masuala yanayoratibu Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu ili kuhakikisha maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yanatekelezwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana jijini Dar es Salaam Katambi amesema, Rais Samia amewataka waandae programu maalumu ya kutengeneza fursa za ajira kwa vijana ambapo itahusisha wizara, wakala na taasisi zote za serikali na sekta binafsi.
Amesema, programu hiyo itahakikisha kuwa kila fedha inayotokana na serikali nchini au tunazozipata kutoka nje ya nchi, iweze kuzalisha fursa za ajira kwa vijana waliojiajili au kutengeneza ajira.
“Tumeanza kufanya upembuzi katika baadhi ya maeneo kwa sasa tatizo la ukosefu wa ajira duniani ni asilimia 13.6 kwa mujibu wa UNESCO ambapo asilimia 75 ya vijana wapo katika ajira ya sekta isiyo rasmi.
“Kwa Afrika na Asia 96% ya nguvu kazi ni vijana, kwa mantiki hiyo tunakusudia kuwezesha sekta binafsi kwa kuwa ndiyo inayoajiri vijana wengi,” alisema Katambi.
Naibu huyo amesema, programu hiyo pia itajikita katika miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ambapo utekelezaji wa miradi hiyo utaweza kuzalisha ajira moja kwa moja na ambazo siyo za moja kwa moja.
Amesema, viongozi wameshaanza mikakati ya mashauriano, vikao vya kikanda na kimataifa vya ajira. Aidha mkakati mwingine ni kuwezesha sekta binafsi, kwa kuwa ndiyo inayoajiri zaidi kwa sekta zisizo rasmi.
Katambi amesema, pia tunaendelea kufanya tafiti za mifumo ili kulegeza masharti ya ukopeshaji, riba za kibenki pamoja na taasisi za maendeleo na mkakati mwingine ambao ofisi iliyonao ni kuzitafuta taasisi na wadau wa maendeleo watakao weza kutoa ruzuku misaada pamoja na fedha zitakazowezesha vijana kujiajiri.
“Aidha ofisi hiyo imejipanga kufuatilia fedha zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana na wenye ulemavu ambapo mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 145.8 zimetolewa kote nchini.
“Serikali hii imetekeleza baada ya kuwezesha vijana kukopesheka katika vikundi lazima ambapo 30% ya zabuni zitakazotolewa katika halmashauri watapewe vijana. Pia mafunzo ya utambuzi na takwimu hii ikiambatana na kuwezesha vijana kupata mikopo, mifuko yetu ya hifadhi ya jamii imeshaanza kutekelezwa,” amesema Katambi na kuongeza. Maelezo yametolewa ili vijana waliopata mafunzo ya uanagenzi 14,134, ambapo serikali ilitumia shilingi bilioni 9 kuwapa mafunzo vijana hao, nao wapewe mikopo katika halmashauri husika ili kuweza kujiajiri.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa