January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Chade atoa maagizo kwa NBAA

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande ameitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kufanya kazi kwa weledi na ushrikiano kwa kuhakikisha inapitia mitaala iliyopo kwajili ya uboreshaji wa taaluma ya uhasibu ili iweze kutoa mchango katika kukuza uchumi kupitia huduma za ukaguzi wa hesabu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati hafla maalum ya kuzindua Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) katika Ukumbi wa APC Bunju, Naibu Waziri ametoa wito kwa wajumbe wapya wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii, uwazi na ushirikiano ili kufanikisha malengo ya NBAA.

Katika hotuba yake, Chande amepongeza uteuzi wa wajumbe wapya wa Bodi, akisema kuwa wamechaguliwa kutokana na sifa stahiki na uzoefu wao katika taaluma ya uhasibu, amesisitiza kuwa Serikali itashirikiana nao kwa karibu kuhakikisha mafanikio ya shirika hilo.

“Serikali kupitia Wizara ya Fedha itatoa msaada na ushauri pale unapohitajika ili kutimiza malengo ya NBAA. Tunaamini uongozi wa bodi hii utaendelea kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika taarifa za fedha kwa sekta binafsi na za umma,” amesema waziri chande

Chande amesistiza umuhimu wa uwazi wa taarifa za fedha katika kuchochea uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi, akieleza kuwa Serikali inatarajia Bodi hiyo kuhakikisha maadili ya kitaaluma yanazingatiwa katika utendaji kazi.

Waziri Chande amebainisha kuwa bodi hiyo mpya inapaswa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya mipango ya shirika ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kibiashara yanayoendelea.

Aidha ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inasimamia vema ujenzi wa kituo jijini Dodoma kupitia kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 29.8 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA Prof. Sylivia Temu amesema wao kama bodi watahakikisha wanafanya kazi ya kusimamia na kukuza tasnia ya uhasibu Nchini ili iweze kutoa mchango stahiki katika kukuza uchumi.