January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri awasihi wananchi kumuunga mkono Mbunge wao

Na Esther Macha,TimesMajiraOnline, Mbarali

NAIBU Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo,Hamisi Mwinjuma, maarufu kama Mwana FA, amewasihi wananchi wa Jimbo la Mbarali kumlinda na kumuunga mkono Mbunge wa Jimbo la Mbarali,Bahati Ndingo.

Mwinjuma amesema  kuwa Ndingo ni mbunge anayefanya juhudi kubwa kutetea maslahi ya wananchi wa Mbarali kwa kusimama kidete Bungeni na kufuatilia changamoto zinazokabili jimbo hilo.

Amesema kuwa wabunge wa aina ya Ndingo wanapaswa kuenziwa na kuungwa mkono ili waendelee kuwatumikia wananchi.

Mwinjuma amesema hayo Novemba 12, 2024,wakati alipofunga fainali za mashindano ya “Bahati Ndingo Cup” yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Highland Estate, Ubaruku, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya. Timu ya Ubaruku iliibuka mshindi wa mashindano hayo na kujipatia zawadi ya shilingi milioni tano.

Akizungumzia zaidi Mwinjuma ameeleza kuwa Mbunge Ndingo ametumia fedha zake kuandaa na kutoa zawadi katika mashindano hayo, hatua inayolenga kuwasaidia vijana kukuza vipaji vyao.

Aidha Mwinjuma amesema kuwa badala ya kutumia fedha hizo kwa familia yake, Ndingo amezitoa kwa ajili ya kuendeleza michezo kwa vijana wa Mbarali.

“Siasa si kazi ya thawabu, malipo yake hutolewa hapa duniani. Kwa hivyo, wananchi wa Mbarali nawasihi muendelee kumuunga mkono Ndingo kwa jitihada zake Haya ni mashindano ya kwanza ambapo mshindi amepata milioni tano, hatua ya kipekee inayoongeza hamasa kwa vijana,”amesema Naibu Waziri Mwinjuma.

Aidha amesema Tanzania, kwa mara ya kwanza, imepata nafasi ya kuandaa mashindano ya mataifa ya Afrika mwaka 2027, kwa kushirikiana na Kenya, chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Baada ya mashindano hayo  Mbunge Bahati Ndingo amesema furaha yake kwa kuona vijana wa Mbarali wakishiriki na kuonyesha vipaji vyao kupitia mashindano hayo.

Amesema ligi hiyo ilihusisha timu 24 zilizoshiriki kutoka kwenye kata mbalimbali za jimbo hilo. Pia, aliahidi kuboresha mashindano hayo katika msimu unaokuja na kuwaomba vijana wasikate tamaa.

Diwani wa Kata ya Rujewa, Jeremiah Michael, amesema  kuwa mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuibua vipaji vya vijana wa Mbarali na kuongeza mapato kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Katika fainali hizo, Timu ya Ubaruku ilitwaa ushindi wa shilingi milioni tano na kombe, huku Timu ya Madibira ikishika nafasi ya pili na kupata shilingi milioni tatu. Zawadi zingine zilitolewa kwa golikipa bora, mfungaji bora, timu yenye nidhamu, na mchezaji bora.