January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri apongeza usimamizi mzuri miradi ya TASAF

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimeneti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Clement Sangu ameeleza kufurahishwa na mafanikio makubwa waliyopata walengwa wa TASAF katika halmashauri ya Manispaa Tabora.

Akizungumza na baadhi ya wanufaika wa mpango huo wa kunusuru kata maskini katika kata za Ipuli na Mbugani katika manispaa hiyo, amesema kuwa mafanikio hayo yamechochewa na usimamizi mzuri wa fedha za mradi huo kwa walengwa.

Amebainisha kuwa lengo la serikali kuanzisha mpango huo wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini zilizotambuliwa ni kuziwezesha kuanzisha miradi midogo midogo itakayowasaidia kujiongezea kipato na kuwa na uhakika wa kupata milo 3.

‘Maeneo yote niliyopita katika manispaa hii nimeelezwa mambo mazuri yaliyofanywa na walengwa wa mfuko huu hususani akinamama, hali inayoonesha wazi kuwa walipata elimu ya kutosha ya matumizi ya fedha hizo’, ameeleza.

Naibu Waziri amefafanua kuwa kupitia mpango huo wanufaika zaidi ya 13,400 katika manispaa hiyo wamejiunga na Mfuko wa Bima ya Afya (CHF), wengine wameboresha makazi yao na wengine wamejiunga na vikundi vya kuweka na kukopa.

Ili vikundi hivyo viwe na nguvu zaidi na endelevu, ameagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya manispaa hiyo kuwapa kipaumbele kwenye mikopo ya asilimia 10 punde itakapoanza kutolewa.

Aidha ameongeza kuwa TASAF imeingia mkataba na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha watoto wote wanaotoka katika kaya maskini ambao watakuwa na sifa za kujiunga vyuo vikuu waweze kupata upendeleo wa kupewa mikopo hiyo.

Kuhusu watoto wanaotoka katika kaya hizo watakaoshindwa kufaulu mitihani ya darasa la 7 au kidato cha 4 amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeanzisha Mradi wa Ufadhili ili kuwawezesha kupata elimu ya Ufundi katika Vyuo vya VETA.

Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeshapeleka takribani sh trilioni 2 ili kuwezesha wananchi kupitia mpango huo wa kunusuru kaya maskini nchi nzima.