November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri ampa miezi mitatu Mkurugenzi VETA

“Naomba ndugu zangu TAKUKURU chunguzeni kwenye maeneo haya ambayo nimeyatolea maagizo, lakini pia kuna maeneo ambayo nimetilia mashaka yachunguzeni na kimsingi tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda sasa kama ni hivyo lazima vyuo hivi vikamilike ili watoto wetu waweze kupata nafasi,”amesema.

Na Doreen Aloyce,TimesMajira Oline-Mafia

NAIBU Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Juma Kipanga ametoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu kuhakikisha ujenzi wa chuo cha VETA wilayani Mafia unakamilika kwa wakati.

Kipanga ametoa maagizo hayo akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo ambapo alitembelea na kukagua ujenzi wa chuo hicho pamoja na taasisi zingine za elimu, hivyo kuonyesha wazi kutoridhishwa na kazi ya ujenzi huo.

Amesema, ujenzi huo ulitakiwa ukamilike tangu Novemba, mwaka jana lakini jambo la kusikitisha hadi sasa bado haujakamilika hivyo alitoa miezi mitatu kuhakikisha mradi unakamilika na wanafunzi wanaanza kusoma.

“Ndugu zangu hapa tatizo kubwa la kuchelewa kukamilika kwa mradi ni kutokana na kazi hizi kuachiwa kwa mafundi ambao hawana uzoefu ,jambo ambalo linakwamisha mradi kushindwa kufikia mwisho,”amesema Kipanga.

Nakuongeza kuwa, “mradi huu unagharimu pesa za kitanzania shilingi bilioni 1.6 ambapo hadi kufikia leo zimeshatumika shilingi milioni 700 na mradi bado haujakamilika hivyo nimetoa miezi mitatu kuanzia leo hii kuhakikisha mradi huu unamalizika na wanafunzi wanaanza kusoma,”amesisitiza Kipanga.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ametoa maelekezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kuhakikisha wanafuatilia changamoto alizoziibua kwenye miradi yote ambayo ametembelea ili kubaini kama kuna ubadhirifu.

Amesema, lengo ni kuona miradi hiyo inatekelezeka kwa wakati ili vijana wanaomaliza elimu ya msingi na hawajabahatika kuendelea wanapata fursa ya kwenda kusoma Chuo cha VETA, lakini hata wale ambao wamemaliza kidato cha sita na wamekosa nafasi ya kwenda mbele na wanatamani ufundi na wenyewe waweze kupata nafasi ya kusoma chuo cha VETA.

“Naomba ndugu zangu TAKUKURU chunguzeni kwenye maeneo haya ambayo nimeyatolea maagizo, lakini pia kuna maeneo ambayo nimetilia mashaka yachunguzeni na kimsingi tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda sasa kama ni hivyo lazima vyuo hivi vikamilike ili watoto wetu waweze kupata nafasi,”amesema.

Amefafanua kuwa, baada ya kukagua chuo na taasisi zingine atakwenda Tanesco ili kuhakikisha umeme unakuwepo na watu wanafanya kazi usiku na mchana ili malengo ya ndoto za Rais Dkt. John Magufuli yatimie.

Pia Naibu Waziri amekemea vikali kitendo cha mkandarasi mmoja kupewa kazi zaidi ya moja hali inayochelewesha kukamilika kwa wakati miradi hiyo ambapo aliwataka wafanyakazi hao kutokuondoka mahali pa pakazi kwani miradi ya Serikali ni ya kimkakati kila kitu kinafanywa kwa malengo.

Mwisho Naibu Waziri Kipanga amepongeza Ofsi ya Udhibiti Ubora wa shule wilaya Mafia kwa kazi ambayo wamefanya kwani wameweza kusimamia ujenzi wa jengo lao na fedha walizopewa na Serikali zimetumika vizuri hadi chenji imebaki na kusisitiza kuwa, wameonyesha uzalendo mkubwa.