December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Katibu Mkuu akikagua kama kifaa kilichofungwa kinafanya kazi. Akionyesha namna kifaa hicho kinavyofanya kazi ni Bwana Afya wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Casto Donald, na pembeni anayeshuhudia ni Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu akagua maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi Mzumbe

Na Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt Evamarie Semakafu, ametembelea Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, kukagua maandalizi ya kupokea wanafunzi tarehe 01 Juni 2020, kufuatia tamko la hivi karibuni la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli la kufungua Vyuo Vikuu nchini, baada ya kuvifunga kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na virusi vya Corona.

Makamu Mkuu wa Chuo akifanya mjumuisho katika wa ziara ya ukaguzi iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu. Wanaoonekana pichani ni baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe na watendaji katika Kituo cha Afya.

Aidha, amekagua maandalizi ya ratiba ya masomo, usajili wa wanafunzi unaoendelea, utekelezaji wa agizo la wizara la kufanya malipo kwa wakati kwa wanafunzi wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Bodi ya Mikopo Tanzania, pamoja na hatua za tahadhari ambazo chuo imezichukua hadi sasa kuwakinga wanafunzi na maambuziki ya Corona.

Naibu Katibu Mkuu Dkt Evamarie Semakafu, akitoa maelekezo ya maboresho baada ya kupokea taarifa na jinsi kituo cha afya kilivyojipanga kuwahudumia wahisiwa wa ugonjwa wa Covid-19. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma Afya Chuo Kikuu Mzumbe Dkt Paschal Songoro, kushoto Bi. Mariam Matao mshauri wa wanafunzi, na katikati Makamu Mkuu wa Chuo na pembeni ni manesi wa kituo hicho.

Dkt Semakafu ameridhishwa na hali katika kituo cha afya kinachotoa huduma, ufungaji wa vifaa vya kunawa mikono kabla ya wanafunzi kuingia madarasani, pamoja na elimu ya jumla inayohusu tahadhari binafsi kwa wanafunzi.

Prof. Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo; amemhakikishia naibu huyo utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kadhalika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto na kwamba kwa zaidi ya asilimia 98% maandalizi yote msingi yamekamilika na tayari wanafunzi wameshaanza kuingia chuoni kwa kuanza masomo Jumatatu 01 Juni 2020.

Hapa ni katika moja wapo ya chumba cha kulala wanafunzi, Naibu Katibu Mkuu akikagua chumba watakacholala wanafunzi kwa kuzingatia nafasi kati ya mtu na mtu.

Dkt Semakafu ameonyesha kuridhishwa na hatua za maandalizi na kupongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Chuo hicho, huku akiwataka elimu zaidi kuendelea kutolewa kujikinga na ugonjwa na hasa kwa wafanyakazi na wahadhiri wa chuo hicho.

Hapa akikagua moja ya vifaa vilivyofungwa kuwezesha wanafunzi kunawa na sabuni na maji tiririka kabla ya kuingia darasani. Eneo hili ni kwenye ukumbi wa mihadhara (lecture theatre) Fanon.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt Evamarie Semakafu, akinawa tayari kuingia ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe alipotembelea kukagua maandalizi ya mapokezi ya Wanafunzi.