April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Katibu Mkuu Nishati aongoza mazishi ya Muhajiri Haule

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. Khatibu Kazungu ameongoza viongozi na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika maziko ya aliyekua dereva wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Tanzania, TANESCO, Muhajiri Haule Mlandizi Mkoani Pwani.

Marehemu Haule alifariki dunia pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo katika ajali ya gari iliyotokea Tarehe 13 Aprili,2025 Wilayani Bunda Mkoani Mara.

Naibu Katibu Mkuu huyo amemuelezea Marehemu Haule kuwa alikua mcheshi na mwenye upendo lakini pia kutokana na uwajibikaji wake alipewa dhamana ya kuwa dereva wa Wakurugenzi watendaji wa Shirika la TANESCO.

“Sisi kama Wizara tumepokea taarifa za msiba huu kwa huzuni kubwa sana, napenda kutumia nafasi hii kwa niaba ya viongozi wangu kutoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu. Mhajiri alikua mtu mwenye upendo na mcheshi hivyo ni vyema kuyaenzi yale yote mazuri aliyofanya enzi za uhai wake, ’’ amefafanua Naibu Katibu Mkuu Kazungu.

Nao baadhi ya wakurugenzi wa TANESCO waliopita waliokufanya kazi na Marehemu akiwemo Dkt. Tito Mwinuka na Maharage Chande wamemuelezea Marehemu kuwa alikua mnyenyekevu na msikivu mwenye hofu ya Mungu.

Miongoni mwa Viongozi wa Taasisi waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji EWURA James Andulile pamoja na chama cha wastaafu UWAWATA

Marehemu Muhajiri Haule alianza kazi TANESCO mwaka 1988 akilitumikia Shirika kwa kipindi cha miaka 37 lakini mwaka 2024 alistaafu kisha kuongezewa Mkataba maalumu.Marehemu Haule ameacha Mke ,Watoto wanne na mjukuu mmoja.