December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi

Nafasi za biashara stendi Dodoma kutolewa kwa njia ya mtandao

Na Zena Mohamed, Dodoma

BAADA ya malalamiko ya wafanyabiashara  wengi jinsi ya kupata  sehemu za kufanyia biashara katika maeneo ya stendi mpya  ya mabasi, eneo la mapumziko Chinangali na Soko jipya, Halmashauri ya jiji la Dodoma imesema  itaanza kutoa fomu za usajili kwa njia ya mtandao.

Hatua hiyo imekuja kufuatia Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi kuanza kutoa maeneo hayo kwa njia ya kujaza fomu kwa njia ya mkono katika eneo la halmashauri ya zamani hali iliyosababisha msongamano wa watu wengi ambao walikuwa wakihitaji kujaza fomu hizo.

Hali hiyo ilimlazimu juzi Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi kufika katika eneo hilo na kusitisha utoaji wa fomu hizo kutokana na mkusanyiko mkubwa ambao aliutaja kuwa unahatarisha maisha kutokana na ugonjwa wa Corona.

Kutokana na hali hiyo ilimlazimu  Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Dodoma Godwin Kunambi  kutangaza kwamba nafasi za maeneo ya kufanyia biashara zitaanza kutolewa kwa njia ya mtandao.