Na Martha Fatael, TimesMajira online, Nairobi
NAFASI ndogo za wanawake ndani ya vyombo vya habari, zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazokwamisha jitihada za kukuza uwezo na kuongeza idadi ya waandishi wanawake katika nafasi muhimu ndani ya vyombo vya habari.
Waandishi wa habari wanawake, wametajwa kuwa na uwezo mkubwa lakini hawapewi nafasi za juu ndani ya vyombo vya habari ili kuweza kushiriki katika kutoa maamuzi na kuwasaidia waandishi wengine wapya wa kike kukua, hali hiyo imejidhihirisha katika mafunzo ya wiki moja nchini Kenya yaliyoshirikisha waandishi wa habari kutoka Tanzania na Kenya na kufadhiliwa na Shirika la Friedrich Naumann Foundation for Freedom.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Ofisa Mipango wa shirika hilo, Veni Swai amesema shirika lake linalofanyakazi zake barani Afrika, liliona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wanawake ili kuwaongezea uwezo wa kushiriki na kujiingiza katika kuomba nafasi za juu ndani ya vyombo vya habari na kusaidia wengine.
“Tulifanya mikutano miwili muhimu sana na kualika waandishi kutoka vyombo vya habari, kilichotushangaza na kutushtua ni kwamba kulikuwa na waandishi wa habari wanawake wachache sana…kati ya waandishi tisa unakuta watatu ama wawili ndiyo wanawake, hii ilisababisha tufanye semina hii ya kutoa mafunzo,” amesema.
Awali akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari hao Mkufunzi, Njeri Kabeberi amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari wanawake kubadilisha mfumo wa ufanyaji kazi kwa kuweka malengo na kutafuta fursa kubwa zaidi ndani ya vyombo vya habari, ili uwezo wao uweze kuonekana.
“Ninachoweza kuwasihi waandishi wa habari wanawake, waongeze jitihada katika kupambania fursa, kuongeza umakini katika kufanya kazi zao ikiwa ni pamoja na kuweka malengo yao, tofauti na yale ya kampuni ambayo wanawapswa kuyafikia kwa pamoja,” amesema.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Joyce Shebe, Tebby Otieno na Chelu Matuzya wamesema mafunzo hayo ni ya tofauti kwani yanawakumbusha waandishi wa habari wanawake, kupambana kutambuliwa kwa kazi zao na kuzikabili fursa.
Wamesema kwa muda mrefu, wanawake wamekua wakikatishwa tamaa kushiriki katika kupambania fursa na nafasi za uongozi kwa kuwekewa vikwazo ama wanaogopa kuthubutu, haya yamekuwa yakiwarudisha nyuma waandishi wanawake.
More Stories
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza