Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema maadili ya uongozi na uwajibikaji ni msingi muhimu wa kujenga sekta imara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Toleo la Pili Jijini hapa leo Juni 25, 2026 uliofanyika katika Hoteli ya Morena, Dkt. Gwajima amesema mwongozo huo umeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha maadili ya viongozi na watendaji wa sekta hiyo.

Amesema miongoni mwa maadili yaliyopewa kipaumbele ni uwazi, uwajibikaji, uaminifu, kutenda bila upendeleo, kuheshimu usiri wa taarifa za wanachama pamoja na kuepuka migongano ya maslahi katika utekelezaji wa majukumu.
“Maadili haya si ya kuwekwa kwenye nyaraka pekee, bali ndiyo msingi wa kujenga imani ya umma, kuvutia ushirikiano wa wadau mbalimbali na kulinda heshima ya sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,”amesema Dkt. Gwajima.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa maadili hayo utasaidia kuongeza ufanisi wa taasisi, kuimarisha ushirikiano kati ya mashirika na Serikali pamoja na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kutoa mchango chanya katika maendeleo ya Taifa.
Dkt. Gwajima alitoa wito kwa viongozi na wanachama wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuutumia mwongozo huo kama nyenzo ya kuimarisha utendaji wao na kuhakikisha wanazingatia misingi ya utawala bora katika shughuli zao za kila siku.
Uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa NaCoNGO Toleo la Pili unalenga kuimarisha mfumo wa uongozi, uwakilishi na uwajibikaji wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Eliakim Maswi amesema kuwa Waziri anataka matokeo kwani wananafasi kubwa ya kujenga Dira ya Maendeleo 2050.
“Mnanafasi kubwa sana ya kutuwezesha sisi kama serikali kutuvadilisha jinsi tunavyoenda na NGo hiz ndani ya nchi,”amesema Maswi.
Naye Mwenyekiti wa NaCoNGO Jasper Makalla awali amesema kuwa waliona changamoto kwenye Baraza na kwenye Sekta wakaomba serikali iwasaidie kuzitatua.
“Tulikuja kwako Mheshimiwa Waziri lakini ulituambia mnamuongozo?,tukasema upo lakini tukaona unamapungufu hauakisi mahitaji ya sasa lakini ulikuwa haupo vizuri na kanuni na sheria.
“Kwahiyo ikaonekana kuna umuhimu wakufanya mapitio ili tuweze kupata toleo ambalo unalizindua leo la 2026,”amesema Makalla.


More Stories
Serikali yazitaka taasisi kujiandaa kukabiliana na El Nino
PPRA yongeza fursa za Makundi Maalum nchini
Mil.80 kujenga stendi ya malori