January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nabii Suguye aridhishwe na miaka mitatu ya Samia

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar

NABII wa Huduma za Kiroho Katika Kanisa la The Word of Recommendation Ministries (WRM) la Kivule Matembele ya Pili Jijini Dar es salaam, Nicolous Suguye amesema ndani ya miaka mitatu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan madarakani ameweza kuonesha uwezo mkubwa wa kuongoza na kulitumikia Taifa .

Nabii Suguye ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 17 ya Kanisa hilo tangu kuanzishwa kwake ambayo yanatarajiwa kufanyika Aprili, Mosi mwaka huu .

Amesema Kanisa la WRM linamuunga mkono kwa asilimia 100 Rais Samia kwa kazi na juhudi mbalimbali ambazo amekuwa akizifanya katika Taifa

“Tupo bega kwa bega na Rais Samia na tunamuunga mkono, kwani ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake ameweza kuonesha uwezo mkubwa wa kuongoza na tumeona matokeo makubwa ndani ya nchi hii, kwani ameweza kuunganisha Tanzania na mataifa mengine jambo ambalo limeweza kuongeza wawekezaji kuja kuwekeza na watalii kuongezeka,”amesema Nabii Suguye na nakuongeza;

” Tumeshuhudia miradi mbalimbali ya kimkakati iliyoanzishwa na Hayati Rais wa awamu ya tano Dkt John Magufuli, ameweza kuteitekeleza kwa wakati pamoja na kuanzisha miradi mingine.”

Akizungumzia miaka 17 ya Kanisa hilo tangu kuanzishwa kwake, Nabii Suguye alisema Kanisa hilo lina mengi ya kujivunia ikiwemo kusaidia jamii kiroho na kimwili.

“Kanisa hili limefanya mengi ikiwemo kusaidia wajane,wazee na watoto yatima pamoja na kufanya juhudi mbalimbali na kuiunga mkono Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara,”amesema.

Amesema Kanisa limeweza kufanya maboresho ya barabara ya kivule na baadaye Serikali iliweza kuwaunga mkono na kuiweka kwa kiwango cha lami pamoja na kutoa vifaa tiba katika hospitali mbalimbali ikiwemo hospital ya rufaa ya kivule.

Aidha alisema katika maadhimisho hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa akimuwakilisha Rais Samia.

“Siku ya Maadhimisho watakuwepo viongozi mbalimbali wa dini na wanasiasa pia kutakuwa na usafiri na chakula bure, ambapo usafiri utaanzia banana kwenda kanisani hakuna gharama yoyote mtu atatozwa,”amesema