January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nabii Joshua aongoza maombi ya saa 74

Waumini wakiendelea na maombi kwaajili ya kuiombea Serikali, Bunge na Mahakama chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala ameongoza maombi ya saa 72 kwa ajili ya kuiombea Serikali, Bunge, Mahakama chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Maombi hayo ambayo yalienda sambamba na kongamano la kihistoria ambalo limewakutanisha maelfu ya watu yamefanyikia Mjini Ifakara ikiwa ni nje ya mji wa Morogoro. Umbali wa zaidi ya kilomita 220 kutoka mjini.

“Mungu ameniita kwa ajili kusudi la kupatanisha, kuunganisha ndiyo maana umeona katika kongamano hili maelfu ya watu waliojumuika ni kutoka pande zote, wapo Wakristo, Waislamu na wasio na imani. Na kwa umoja wetu tumesimama kuiombea Serikali, Bunge, Mahakama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

“Tumeziona baraka kubwa kutoka kwa Mungu, mamia ya watu wameokoka, wameponywa na kufunguliwa katika vifungo mbalimbali mbalimbali,”amesema Nabii Dkt.Joshua.

Ameongeza kuwa, ameamua kusimamia maombi katika mihimili hiyo muhimu kwa sababu anaamini kuwa, Mungu akizisimamia kwa ufanisi Taifa litazidi kustawi kwa kasi katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, kijamii na kisiasa.

Nabii Dkt.Joshua amesema, Kampeni ya Kuliombea Taifa ya ‘Pray for Nation’ aliyoiasisi miaka kadhaa iliyopita inaendelea mji baada ya mji, wilaya baada ya wilaya na mkoa baada ya mkoa.

Huduma ya Sauti ya Uponyaji yenye makao yake makuu Yespa, Kihonda mjini Morogoro iliasisiwa miaka kadhaa Mjini Morogoro ambapo licha ya kuwa baraka kwa kuwafungua maelfu ya watu katika vifungo vya shetani imekuwa mstari wa mbele kusaidia huduma mbalimbali za kijamii, kupatanisha na kuunganisha watu kutoka pande mbalimbali ikiwemo kuwakabidhi viongozi wote kwa Mungu kupitia maombi ya kila siku.

Maombi yanaendelea