May 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Na Israel Mwaisaka,Rukwa

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali,ameitaka Bodi ya maji Bonde la Ziwa Tanganyika, kuhakikisha jitihada zinazofanyika za kuhifadhi Bwawa la Mfili kama chanzo kikuu cha maji katika mji wa Namanyere,ziendane na utunzaji msitu wa Mfili ambacho ndio chanzo kikuu cha maji katika bwawa hilo.

Lijualikali,amezungumza hayo kwenye mkutano wa wadau kwa ajili ya utambulisho wa uhifadhi wa Bwawa la Mfili,ambapoamewataka viongozi wa vijiji na vitongoji, wanaouzunguka msitu huo kuwa mstari wa mbele kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa msitu wa Mfili kama chanzo cha bwawa hilo.

Amesema,viongozi wa vijiji,vitongoji na kata jukumu lao la msingi ni kulinda hifadhi ya mazingira katika maeneo yao, na kuhakikisha wanaovamia vyanzo vya maji wanadhibitiwa mapema badala ya kusubili kabla hawajaingia ndani ya hifadhi na kujenga,hali ambayo ameeleza kuwa inaipashida Serikali kuwaondoa katika maeneo hayo.

“Siyo jambo jema kuanza kuwaondoa watu kwa njia ya oparesheni, wakati viongozi wa vijiji na kata mngeweza kulidhibiti tatizo hilo kwa wakati,”amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,Pankrasi Maliyatabu,amesema suala la uhifadhi wa mazingira na kulinda chanzo cha maji cha Mfili kinahitaji utashi wa kisiasa, kwa viongozi wa kisiasa na kujitahidi kusema ukweli kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi chanzo cha maji.

Amesema kuwa,suala la uhifadhi wa mazingira halihitaji maneno ya kufurahisha bali ni kueleza ukweli na kila mmoja aweze kujua kwamba kutohifadhi vyema mazingira kutasababisha majanga na tatizo la maji.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Ziwa Tanganyika Mhandisi Odemba Cornel, amesema kuwa shughuli za kibinadamu kwenye chanzo chochote cha maji ni hatari,hivyo kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha chanzo cha maji hakiingiliwi ili kulinda Bwawa la Mfili na watu waweze kupata maji wakati wote.