Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Mzumbe
RAIS Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Uongozi na Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu ya Morogoro.
Rais Samia alitunukiwa Shahada hiyo ya Uzamivu ya udaktari wa heshima leo Novemba 24,2024,mkoani Morogoro katika mahafali ya 23 yaliyofanyika chuoni hapo.
Kabla ya shahada hiyo, Rais Samia, alikuwa amekwishatunukiwa shahada zingine za uzamivu tano za udaktari wa heshima katika fani mbalimbali na vyuo vikuu kutoka ndani na nje ya nchi.
Vyuo vingine vilivyowahi kumtunuku Rais Samia Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Heshima ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki na Chuo Kikuu cha Anga nchini Korea.
Akizungumza sababu za kumtunukia shahada hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amesema Rais Samia amekuwa kielelezo cha uongozi ndani na nje ya nchi.
Profesa Mwegoha amesema shahada hiyo inakuwa ya kwanza kutolewa na chuo hicho tangu kuanzishwa kwake.
Mkuu wa Kampasi ya Mzumbe Dar es Salaam, Profesa Cyriacus Binamungu, ameeleza kwa kina sababu ya Rais Samia ya kumtunuku shahada hiyo.
Kwa mujibu wa Prof. Binamungu hadi wanafikia uamuzi huo, walipitia kwa makini katika muktadha wa misingi ya uanzishwaji wa chuo hicho na kubaini kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia anastahili shahada hiyo.
“Shahada hii ni kielelezo katika kutambua mchango wake (Rais Samia) kwenye jitihada za maendeleo endelevu ya Tanzania na nje ya nchi kwa ujumla,” amesema.
Amesema Rais Samia ameweka historia ya kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke na baadaye kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini.
Amesema katika uongozi wake mafanikio mbalimbali yamefikiwa na ndiyo yanayofanya astahili shahada hiyo ya udaktari wa heshima.
Profesa Binamungu, amesema wameangalia uongozi wa Rais Samia tangu akiwa na nafasi nyingine hadi alipokuwa Rais.
Amesoma wasifu wake akigusia mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali chini ya Rais Samia katika sekta za afya, elimu, miundombinu, diplomasia, uchumi na demokrasia.
Amwongeza kuwa ndani ya uongozi wake, Rais Samia ameanzisha falsafa ya 4R iliyojenga msingi wa utawala bora na kuzaa tume ya haki jinai na kikosi kazi.
“Kwa ufupi sana haya ni baadhi ya mambo yaliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Hatuna shaka kwamba mtunukiwa wetu amejitanabaisha kwamba yale mafunzo anayatumia vema katika kujenga ustawi wa Watanzania,” amesema Profesa Binamungu.
Awali, akitoa salamu za wizara, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aliipongeza seneti ya chuo hicho kwa uamuzi wa kikanuni wa kutoa shahada hiyo kwa Rais Samia.
Alimpongeza Rais Samia kwa kutunukiwa shahada hiyo, amesema anastahili kutokana na uongozi wake wenye maono ya mbali, sahihi na kuwapeleka watu katika njia sahihi.
Amesema katika uongozi wake baada ya kuapishwa alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na kueleza kila anachotaka katika kila wizara.
Ameeleza katika wizara ya elimu alielekeza mageuzi ya elimu, jambo ambalo mwaka mmoja baadaye dunia ikaanza kuzungumzia mageuzi hayo.
Amesema mwaka huu Umoja wa Afrika (AU) imeutambua kuwa mwaka wa mageuzi ya elimu, hivyo maono ya Rais Samia yalitangulia kabla ya ulimwengu.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Saida Yahya Othman, alisema tunuku ya shahada ya heshima ni tukio la kipekee kwa mtunukiwa na mtunuku.
Amesema hiyo ni tunuku ya kwanza kwa chuo hicho, pili inakwenda kwa Rais wa Tanzania, ambaye pia ni muhitimu wa chuo hicho.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 5,012, wamehitimu kati yao wanawake ni 2,354 na wanaume ni 2,358 karibu asilimia 50 kwa 50.
Kwa mujibu wa
Kwa mujibu wa Pfof. Mwegoha katika mahafali hayo ya 23 kuna wahitimu 12 wa shahada za uzamivu, ikiwa ni idadi kubwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu