January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mzee miaka 60 adaiwa kumbaka mtoto wa miaka 5

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Pemba

MZEE wa miaka 60 Mkazi wa shehia ya Finya Wilaya ya Wete amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba akituhumiwa kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano.

Mzee huyo anafahamika kwa jina Haroub Abdalla Hamad pia anatuhumiwa kumfanyia udhalilishaji mkubwa wa kijinsia mtoto huyo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kesi hiyo ilisomwa katika Mahakama ya Wilaya ya Wete chini ya Hakimu wa Mahakama hiyo Rashid Magendo ,kwa kuwa Hakimu wa Mahakama ya Mkoa alikuwa nje ya Mahakama kikazi.

Imedaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashitaka wa Serikali Mohammed Said Mohammed kwamba mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo tarehe isiyofahamika ya mwezi 10/2020 baina ya saa 6;30 mchana na saa 11;00 jioni huko Bahren Finya.

Amesema kwamba siku ya tukio , bila ya ridhaa yake alimbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano (jina linahifadhiwa) ikiwa ni kinyume na kifungu cha 108 (1) ,(2) ,na kifungu cha 109 (1) cha sheri ya adhabu namba 6/2018 sheria za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwendesha mashataka ametaja kosa lingine mbadala (Altanative Count) la udhalilishaji mkubwa wa kijinsia kinyume na kifungu cha 139 (1),(a) ,(2),(b) ccha sheria namba 6/2018 ,sheria za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Mheshimiwa hakimu shauri hili limekuja kwa ajili ya kutajwa , lakini lilistahili kusikilizwa katika mahakama ya mkoa,tunaomba upange tarehe nyingine”alishauri.

Hata hivyo mtuhumiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za aina hiyo , na mtuhumiwa amepelekwa rumande hadi Novemba 12,mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kutajwa katika mahakama ya mkoa.