Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
KATIKA kuhakikisha changamoto ya ajali za barabarani hasa kwa watoto zinapungua nchini, ipo haja ya Serikali kufanyia mabadiliko Sheria ya usalama barabarani huku Wizara ya Mambo ya Ndani chini ya Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani kinasimamia na kuzisisitiza.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Habari na Mahusiano wa Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza (MYCN) Paschal Charles wakati wa kikao cha wanahabari, watoto na Maofisa wa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani kilichofanyika Jijini Mwanza kupitia mradi wa usalama wa mtoto barabarani.
MYCN waliamua kuja na mradi wa usalama wa mtoto barabarani ambao umejikita katika kuchochea mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2002, lakini licha ya mabadiliko hayo ya sheria bado imesahau sana uwepo wa watoto hasa katika matumizi ya barabara na vyombo vya usafiri.
Charlse amesema, kwa kuliona hilo katika sheria kuna vipengele tofauti tofauti na kama shirika waliangazia maeneo manne ambayo mtoto amesahaulika ikiwemo matumizi ya viti maalumu vya watoto katika vyombo vya usafiri, kofia ngumu, ufungaji wa mikanda pamoja na utambuzi wa mtoto kama abiria.
Amesema kuwa, ni wakati wa serikali kubadilisha sheria hiyo na kuangalia suala la matumizi ya viti maalumu vya watoto kwenye vyombo vya usafiri kwa upande wa pili kwani nchi sasa inabadilika katika matumizi ya miundombinu na vyombo vya moto.
“Kwa utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani(WHO), 2018 umebaini kuwa viti hivyo vinapotumiwa kwa usahihi vinaweza kusaidia mtoto pindi ajali inapotokea kwa asilimia 75 na asipo tumia kuna asilimia 25 tu ya kupona katika ajali hivyo jamii na Serikali inawajibu wa kuiga tabia hii ya matumizi ya viti hivyo kwa watoto hivyo ni vema kufanya mabadiliko haya kwani sheria inaweza kuwekwa lakini usimamizi wake ukiwa mbovu na usipo kuwa thabiti malengo yaliotazamiwa hayatoweza kufikiwa,” amesema Charles.
Kwa upande wa matumizi ya kofia ngumu (helement) amesema, watoto wamekuwa ni miongoni mwa watumiaji wa pikipiki kupelekwa shuleni na maeneo mbalimbali hivyo utakuta abiria mtu mzima ndio ananufaika na kofia hizo na mtoto anabaki bila kofia hivyo endapo ajali ikitokea mhanga mkubwa ambaye anaweza kupata majeraha makubwa zaidi ni mtoto.
Kuhusu suala la utambuzi wa mtoto, sheria hiyo inayotumika sasa inaeleza ili mtoto aonekane kama abiria inabidi awe na miaka 12 na kuendelea lakini wakiwa chini ya umri huo mpaka wawe wawili ndio wanatambulika kama abiria mmoja, maisha na uhai ni wa mtu mmoja siyo ya watu wawili ndio maana wanalizungumzia jambo hilo ili kuona sheria inabadilishwa kwa kujali uhai na maslahi ya mtoto.
“Tulikutana na changamoto kubwa sana hususani katika ajali ambazo zimekuwa zinaendelea hasa upande wa watoto vifo vinaongezeka wanatokea kugongwa katika maeneo ya barabara, mwaka jana tulishuhudia ajali iliotokea mkoani Arusha ya watoto wengi ambao walitia simanzi katika nchi yetu, kwa kuliona hilo kama shirika tuliamua kuja na mradi huo wa usalama wa mtoto barabarani ambao umejikita katika kuchochea mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani kwa kuiomba Serikali kufanyia mabadiliko,”.
“Kwa takwimu za WHO inaonesha kila mwaka watu milioni 1.35 hupoteza maisha kwa ajali za barabarani na kila sekunde 24 mtu mmoja hupoteza maisha hutokea mara tatu zaidi katika nchi zinazoendelea kuliko zilizoendelea, chanzo namba moja ya vifo vya watu wenye umri kuanzia miaka 5-29 pia ni chanzo namba 8 ya vifo vya watu Duniani,” amesema Charles.
Baadhi ya wanahabari watoto walio chini ya MYCN wakiwemo Alfred Anthony, Mariam Daud na Rehema Juma walitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kufanyia mabadiliko sheria ya usalama barabaraji kwa kumjali mtoto sanjari na kutoa elimu kuhusu vizuizi vya watoto katika vyombo vya usafiri kwa maana ya kuwekwa mikanda inayoendana na watoto kwani sheria ilipo sasa inamapungufu katika suala zima la mtoto awapo barabarani na kwenye vyombo vya usafiri.
Wamesema, ajali nyingi utokea kutokana na uzembe wa madereva, mwendo kasi, matumizi ya simu wakati akiendesha chombo cha moto, kutozingatia alama za barabarani ikiwemo kwenye taa au alama ya pundamilia (kivuko cha watembea kwa miguu) zinazoashiria gari kusimama ili watu wapite wao uongeza kasi zaidi, uzidishwaji wa mizigo katika gari la abiria pamoja na watoto kutofuata utaratibu wa kuvuka barabara katika vivuko vya watembea kwa miguu.
Maofisa wa Kitengo cha Elimu ya usalama barbarani Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza CPL Dismas Temba na PC. Charlse Munthal wamesema, inaonesha sheria imewasahau sana watoto na kuona kama siyo watumiaji wa barabara ambapo vyanzo vikuu vya ajali barabarani ni mwendo kasi ambao umechukua maisha ya watu wengi ikiwemo watoto ambapo takwimu za WHO zinaonesha ajali hizo kwa nchi za Afrika zimekuwa zikichukua maisha ya watu.
Chanzo kingine ni ubovu wa miundombinu ya barabara, ubovu wa chombo cha usafiri, ‘over take’ na hali ya hewa ambapo unakuta mvua inanyesha na kusababisha maji kujaa barabarani lakinj dereva analazimisha kuendelea na safari hivyo waliwahimiza watoto hao pamoja na jamii kwa ujumla kutokubali dereva kuendelea na safari wakati mvua zinanyesha kwani kama wao hawaoni mbele wala alama za barabarani hata dereva ni hivyo hivyo pia haoni.
Mbali na changamoto hizo zinazopelekea kutokea kwa ajali, wametoa wito kwa wazazi na jamii kuhakisha watoto hawavuki barabara bila ya kuwa na uangalizi wa mzazi hata katika maeneo ya taa ya kijani inayosema nenda wakati ni salama pamoja na watoto kuvuka katika kivuko cha watembea kwa miguu hata kama kipo mbali na shule kwani vinawekwa kulingana na wataalamu hivyo ni vyema watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia na kutii sheria ya usalama barbarani.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito