November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Mstaafu Job Lusinde

Mwili wa mwanasiasa mkongwe balozi Lusinde kuwasili Dodoma kesho

Na Doreen Aloyce,Timesmajiraonline

MWILI wa aliyekuwa mwanasiasa Mkongwe na waziri pekee aliyebaki katika Baraza la Mawaziri la kwanza baada ya nchi kupata Uhuru Balozi Mstaafu Job Lusinde unatarajiwa kuwasili kesho mkoani Dodoma.

Marehemu Mzee Lusinde amefariki dunia leo alfajiri katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo Jijini Dar es Salaam alipokuwa anapatiwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake leo Jijini Dodoma,msemaji wa familia mbaye ni Waziri Mkuu Mstaafu mzee John Malecela amesema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake Jijini Dodoma.

Akimzungumzia marehemu enzi za uhai wake mzee Malecela amesema alikuwa ni kaka yake na atakumbukwa kwa utendaji kazi uliotukuka,uzalendo kwa nchi yake kupitia nafasi mbalimbali alizozitumikia.

Enzi za uhai wake marehemu Mzee Lusinde aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Mkoa wa Dodoma, ambapo mjumbe wa baraza hilo Mzee Peter Mavunde amemuelezea kuwa ni mtu aliyekuwa mwaminifu kwa chama na Serikali yake.

Kwa upande wake mbunge wa Dodoma Mjini Anton Mavunde ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana amemuelezea mzee Lusinde kama mtu aliyechangia yeye kuwa mbunge kutokana na ushauri wake alioutoa kwake.

Marehemu Lusinde alizaliwa septemba 1930 pamoja na nafasi nyingine katika baraza la mawaziri,pia amewahi kuwa balozi nchini China, alikuwa mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma(DUWASA) na ameacha mke na watoto wanne.