Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
POLISI wilayani Igunga Mkoani Tabora limekamata watu 13 akiwemo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Mwalimu wa shule ya msingi na Mtemi wa sungu-sungu na kuwafikisha katika mahakama ya Hakimu Mfawidhi wilayani hapa kwa tuhuma za mauaji ya wafugaji 3 wakazi wa kata ya Isakamaliwa.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi wilayani hapa Elmajidi Kweyamba alitaja walioshitakiwa mbele ya hakimu wa wilaya Lidia Ilunda kuwa ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Isakamaliwa Shija Mboje (48) na Mwalimu wa shule ya msingi Isakamaliwa Michael Masanja (36).
Wengine ni Jijadi Katambi (43) ambaye ni Mtemi wa Jeshi la Jadi (sungu-sungu) kata ya Isakamaliwa, Maleba Machenge (37), Ngoga Ifegelo (50), Ndulu Manyenye (32), Shakali Ifegelo (30), Magembe Mwandu (25), Mahona Jilala (35), na Bakari Hamis (45).
Wengine ni Kulala Shigela (38), Masunga-Kulwa (39) na Nkwabi-Mipawa (58) wote wakazi wa kata ya Isakamaliwa.
Majid alibainisha shitaka la kwanza linalowakabili kuwa ni la Mei 12, 2022 majira ya saa 8 mchana katika Kijiji cha Isakamaliwa, kata ya Isakamaliwa ambapo watuhumiwa wakiwa na nia ovu walimuua Darushi Bukwere (26) mkazi wa kata ya Isakamaliwa kwa makusudi.
Shitaka la pili ni la mauaji ya Gwisu-Manyenye (30) mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa lililotendeka Mei 12, mwaka huu katika kata hiyo hiyo.
Majid aliiambia mahakama kuwa shitaka la 3 linalowakabili ni la mauaji ya Jacob Tungu (32) mkazi wa kata hiyo hiyo.
Alisema washitakiwa wote walitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 196 kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kesi hiyo imeahirishwa hadi hadi Machi 30, mwaka huu itakapotajwa tena, washitakiwa wote wamepelekwa mahabusu.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango