Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt.John Magufuli kwa kutoa hotuba fupi bora jana, yenye mwelekeo wa kuendelea kuipaisha Tanzania zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kiboye ametoa pongezi hizo wakati akizungumza leo Agosti 7,2020 mkoani hapa kuelezea juu ya namna ambavyo hotuba ya Rais Dkt. Magufuli baada ya kupokea fomu ya kuwania urais kwa awamu ya pili kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dodoma jana ilivyokuwa imejaa mambo ya msingi kwa mustakabali wa Taifa letu.
Amesema, hotuba ya jana ilikuwa na mashiko na imegusa Watanzania wengi, hivyo wataendelea kumuombea ili Oktoba 28, mwaka huu akaandike historia kubwa kupitia ushindi wa kishindo.
Jana wakati Rais Dkt.Magufuli ambaye ni mgombea wa kiti cha urais na anayetetea kiti chake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu katika ofisi za NEC jijini Dodoma alisema,ameamua kuchukua fomu yeye na Mgombea Mwenza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi kingine cha miaka mitano ili wakamilishe miradi mingi ya maendeleo waliyoianza awali.
Pia alisema,katika kipindi chake cha miaka mitano umeme umesambazwa katika vijiji 9,402 kutoka vijiji 3,000 wakati wanaingia madarakani na vimebaki vijiji 3,000 ambavyo alisema havitamshinda kuvifikia kwa miaka mitano.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea