February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti CCM, Mbunge Rorya wavuruga mafunzo ya makatibu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

JOTO la Uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), linazidi kupana huku mafunzo kwa watendaji wa chama hicho tawala yakivurugwa.

Hatua hiyo inatokana na tukio la kustaajibisha lilotolea juzi katika mafunzo ya watendaji amapo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Ongujo Wakibara kwa kushirikiana na mbunge wa Jimbo hilo, Jafari Chenge wakiyavuruga na kumwaga hongo kwa wajumbe wa mafunzo hayo.

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika juzi Mbunge Chege na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Ongujo Wakibara ambao wanadaiwa waliingilia semina ya makatibu wa matawi na kata iliyofanyika Februari 20, 2025 ambapo viongozi hao wanadaiwa kugawa posho kiasi cha Shilingi 50,000 kwa kila katibu aliyehudhuria mafunzo hayo.

Tuko hilo ambalo liliibua mjadala katika makundi sogozi ya mitandao ya kijamii (WhatsApp ya CCM Mkoa wa Mara) ilidai kuwa utaratibu huo unakiuka maelekezo kutoka makao makuu ya CCM Taifa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mafunzo hayo ya watendaji yasiingiliwe na viongozi au wanasiasa kwa sababu ni mafunzo ya kiutendaji na chama kilisema kitagharamia kila kitu ikiwemo chakula na posho.

“Lengo la chama kufanya hivyo ilikuwa ni kuondoa urasimu wa wagombea kutumia nafasi hiyo kutoa rushwa kinyume chake Mwenyekiti wa chama na mgombea wake ambaye ndiye mbunge kwa sasa wamevamia ukumbi na kutoa posho hizo.

“Jambo hili halijawafurahisha hata wakufunzi haswa kauli za Mwenyekiti na Mbunge baada ya kuzuiwa na wakalazimisha kufanya kwa nguvu,” alisema sehemu ya taarifa.

Gazeti tando la George Marato Tv, imefatilia taarifa hiyo na kuzungumza na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafar Chege kwa njia ya simu na kudai yupo msibani toka asubuhi na hajaudhuria kikao hicho na kushangazwa na taarifa hiyo.

Hata hivyo Chege alikili kuiona taarifa hiyo kwenye makundi sogozi ya CCM lakini hajui lengo lake.

“Nimeshangazwa na taarifa hiyo mimi nipo msibani na nimeambiwa kikao hicho kimeenda vizuri na kimalizika salama hizo taarifa ni za uongo,” alisema Chege.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Ongujo Wakibara hakuweza kupatikana kwenye simu na jitihada za kumtafuta kuzungumzia jambo hili zinaendelea.

Hata hivyo pamoja na hali Mwenyekiti huyo wa CCM anadaiwa amekuwa akiwasimamisha viongozi ovyo ovyo ambapo hivi karibuni katika Kata za Mkoma, Kirogo, Kinyenche, Nyathorogo, Goribe na Tai aliwasimamisha vongozi wa matawi bila kuihusisha kamati ya siasa.