Na Irene Clemence,TimesMajira Online,Dar
MWENYEKITI wa Bodi ya Benki ya Afrika Dkt.Nyamajeje Calleb Weggoro,ameanza kutekeleza mkakati wa kuendeleza benki kwa kutembelea matawi makubwa mawili.
Matawi aliyotembelea ni Business Center Oysterbay moja ya tawi ambalo ni kituo kikubwa cha kutoa huduma kwa wateja wa makampuni na biashara, mwenyekiti alitembela pia tawi la Victoria lililopo kijitonyama.
Ziara hii inakuja baada ya mwenyekiti kukutana na uongozi na wafanyakazi wa benki hiyo katika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo kwenye jengo la NDC ambapo walijadiliana masuala mbalimbali yanayohusiana na kuboresha uendeshaji wa benki kwa ufanisi zaidi.
Dkt.Weggoro ametembelea matawi kuelewa shughuli za benki katika kusaidia maendeleo ya nchi na mchango wake katika kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha hususani kipindi hiki ambacho Tanzania imeingia katika uchumi wa kati.
Benki hiyo imeonekana kuwa thabiti katika kufanikisha uwekezaji uliofanywa nchini Tanzania na imeshiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo tangu 2007.
Pamoja na ushiriki wa benki hiyo katika miradi mbalimbali ya maendeleo, benki imeonyesha dhamira yake katika kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) kwa kubuni bidhaa na huduma za kuvutia wateja.
Kama benki ya biashara, benki inayo wateja waliogawanywa katika makundi ya wateja wa Rejareja, Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) na wateja wa Makampuni.
Kabla ya kujiunga na Benki ya Africa Tanzania Limited, Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro,aliteuliwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kati ya mwaka 2016 hadi 2019 ambapo alifanyakazi kwa weledi mkubwa akisimamia maslahi ya nchi nane: Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Rwanda, Eritrea, Visiwa vya Shelisheli, na Sudan Kusini. Dkt.Weggoro pia aliteuliwa kama Msaidizi na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ushirikiano wa Kikanda na Masuala ya Uchumi), 2013-2016.
Kwa sasa amejiunga na timu ya Benki ya Afrika Tanzania kusaidia kuendeleza mipango na mikakati yake ya maendeleo na kuifikisha kwenye viwango vya juu kutokana na uzoefu na utaalamu wake mkubwa katika fani mbalimbali zikiwemo uongozi, uchumi, fedha, upangaji na utawala, uhandisi wa viwanda, upangaji wa miradi na kujengea uwezo tasisi.
Kwa njia nyingi Dkt. Weggoro amehusika kuleta mabadiliko ya nchi mbalimbali za Kiafrika kupitia kushiriki kwake katika mipango ya maendeleo katika nchi alizowakilisha.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25