May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti ACT Wazalendo afanya ziara mkoani Dar

Na Mwandishi wetu,timesmajira

Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amefanya ziara maalum ya siku moja ya kuwafariji wananchi wa Maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Ziara hiyo ambayo ni mwendelezo wa desturi na ada ya Mtangulizi wake (Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad) ya kila Mwaka, inayolenga kuwafikia watu, hasa ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambayo imeanza mapema leo mara tu Mwenyekiti Othman alipowasili Jijini hapa, akitokea Zanzibar.

Akiwa katika Kituo cha majumuisho ya ziara hiyo, huko Msasani ‘Maandazi Road’ (Bonde la Mpunga), Othman amesema, ndani ya ramadhan kuna mafunzo mengi mazuri ambayo watu wote wema wanayahitaji ili kuendeleza ubinadamu hapa Duniani, ambao ni katika misingi muhimu ya maendeleo ya jamii, nchi na taifa kwa ujumla.

Naye, Mmoja wa watu waliotembelewa na Mwenyekiti huyo,Rugemalira wa Kigamboni, ameeleza faraja kubwa ambayo ameipata, kwake na kwa wananchi, kutokana na kufikiwa na viongozi wa kitaifa, pamoja na azma njema katika kutekeleza kile kinachoonekana .

Amesema ni jitihada za kuwatatulia changamoto zao.

Katika Ziara yake hiyo, Othman amewatembelea na kuwajulia hali viongozi, wagonjwa na wazee mbalimbali wasiojiweza, wakiwemo wa mitaa ya Kigamboni, Mbagala Rangi Tatu, Temeke Azimio, Tabata Segerea, Magomeni na Msasani, katika Jimbo la Ubungo amefika ndani ya Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni.