December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa Uhuru wazindua miradi ya Bilioni 40.9 Ilala

Na Heri Shaaban , TimesMajira Online

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amesema MWENGE wa UHURU umezindua miradi ya maendeleo shilingi Bilioni 40.9 Wilaya Ilala .

Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo ,alisema katika miradi hiyo iliyozinduliwa na Kiongozi wa Mwenge Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mzava ikiwemo Shule ya Sekondari Minazi mirefu Ukonga,Mradi wa Usambaji Maji Bangulo,Kituo cha afya cha Kisasa Kinyerezi, Kituo cha Polisi Mwanagati,Barabara ya Tukuyu kata ya Ilala, watoto wenye Mahitaji maalum kata ya Upanga .

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa UHURU mwaka 2024 Godfrey Mzava aliwataka Wananchi wa Wilaya ya Ilala kutunza vizuri miradi hiyo ya Maendeleo ya Serikali ikiwemo Kituo cha Afya cha Kisasa kilichopo Kinyerezi.

KIONGOZI wa Mwenge Mzava aliwapongeza Madiwani wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, wakiongozwa na Meya Omary Kumbilamoto, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo na Mkurugenzi wa jiji Jamary Mrisho Satura kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo vizuri ambapo aliwataka wananchi wa wilaya ya Ilala kutunza miradi hiyo.

Akisoma Risala ya Mwenge wa UHURU ya mwaka 2024 Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Ilala Flora Mgonja, alisema baadhi ya mambo yaliyotekelezwa Wilaya ya Ilala shilingi milioni 260 katika maswala ya Afua na Lishe ,mwaka 2023 /2024 TAKUKURU Ilala ilitoa elimu ya Kupambana na Rushwa kwa watumishi, Madiwani, ili wasimamie miradi ya maendeleo ya Serikali ambayo imetekeleza katika kata zao .

Kaimu Katibu Tawala Frola Mgonja alisema Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Serikali wanalinda misitu wa Nyuki Kinyerezi na Mzinga pia wananchi 600 wamepewa elimu ya Kilimo cha kisasa.

Aidha Flora Mgonja alisema mikakati ya Serikali kujenga hospitali ya kisasa Kisukuru na Minazi mirefu kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Zaituni Hamza, alisema kata ya Kinyerezi wanayo furaha kubwa kupokea Mwenge wa UHURU mwaka 2024 chini ya Kauli Mbiu isemayo Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi Serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu ambapo alisema kituo cha afya Kinyerezi ni miongoni mwa vituo 33 vya kutolea huduma za afya katika halmashauri hiyo.

Dkt Zaituni Hamza alisema mwaka 1976 kilianza kutoa huduma kama zahanati ya kawaida ambapo ongezeko kubwa la wananchi pamoja na idadi ya wananchi zahanati hiyo ilishindwa kumudu wagonjwa hususan wamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

“Kutokana na ongezeko la wananchi na wagonjwa kuwa wengi hali hiyo imepelekea halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Mkurugenzi wa jiji Jamary Mrisho Satura kuanzisha ujenzi wa majengo manne ambalo ni jengo la upasuaji, wodi ya Wazazi, Mahabara jengo la wagonjwa wa nje, ili kuipandisha hadhi iliyokuwa zahanati na kuwa kituo cha afya Kinyerezi”alisema Zaituni.