December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa Uhuru 2024 kuzimwa Mwanza

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kuwasili Oktoba 6, mwaka huu, ambapo umekuwa ukikimbizwa nchini kwa miaka 60, utapokelewa katika Kijiji cha Nyamadoke, Buchosa, wilayani Sengerema, ukitokea Geita.

Mtanda amesisitiza umuhimu wa tukio hilo, Oktoba 1,2024,kuwa ni heshima kubwa kwa Mwanza kuzima Mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilometa 627 katika Halmashauri nane za wilaya zote saba, mkoani Mwanza,na utaweza kuweka mawe ya msingi, kukagua, na kuzindua miradi 58 yenye thamani ya sh. bilioni 99.2.

Katika taarifa yake, Mtanda amebainisha vyanzo vya fedha zitakazotumika na zilizotumika katika miradi hiyo.Ambapo. bilioni 2.6 ni michango ya wananchi, na bilioni 2.7 kutoka halmashauri,bilioni 19.7 kutoka Serikali Kuu, na bilioni 74.2 kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Kilele cha mbio za Mwenge kitafanyika Oktoba 14,2024,ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, tukio ambalo litakumbusha miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, na litajumuisha ibada maalumu itakayofanyika katika Parokia ya Nyakahoja, kuanzia saa 12 hadi saa 2 asubuhi , ikiongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, Askofu Renatus Nkwande.

Pia, wiki ya vijana itafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 13, ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, atakuwa mgeni rasmi na litafanyika kongamano la vijana wajasiriamali na wanufaika wa mikopo ya serikali kuonesha shughuli zao na ubunifu.

Aidha wananchi pia wanakaribishwa kushiriki katika mbio ndefu (Marathon) zitakazofanyika kwa ushirikiano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), ambapo washindi wa mbio hizo watapata zawadi mbalimbali,hivyo, Mtanda amewasisitiza wananchi kuwa na uzalendo na kuonyesha ushirikiano katika tukio hili la kihistoria.