November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mweli : Maandalizi ya Mkutano AGRF yanaenda vizuri,Marais kadhaa kuthibitisha kuhudhuria

Na Prona Mumwi, timesmajira

Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Gerald Mweli amesema hadi sasa Marais kadhaa wamethibitisha kushiriki mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) utaofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa upande wa Mawaziri zaidi ya asilimia 80 ya matarajio wamethibitisha kushiriki kwenye mkutano huo.mkubwa na usajili unaendelea mpaka baadae hii leo.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati maandalizi ya mkutano huo yakiendelea Mweli
amesema, mpaka sasa nchi imeshavuka lengo la washiriki ambapo lengo lilikuwa ni kufikisha washiriki elfu tatu lakini hadi sasa waliojiandikisha wamezidi na kufikia elfu 4 hivyo wanatarajia kufunga dirisha la usajili leo Agosti 29, 2023.

“Idadi hii ya washiriki inaonesha imani yao kwa nchi yetu, lakini kufikia jitihada hizo ni juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuitangaza nchi kimataifa. Hivyo nitoe rai kwa watu wote wakiwemo wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mkutano huu wa AGRF kwani watapata manufaa makubwa.” Ameeleza Mweli

Amesema Serikali imealika kampuni kubwa zinazojihusisha na kilimo ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara nchini watakaotangaza biashara zao kimataifa.

Aidha, Mweli ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kufungua kiwanda cha kuchakata mbolea kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi, ambapo kupitia mkutano huo wa Mifumo ya Chakula 2023 kiwanda hicho kitatangazwa ili kupata soko la Kimataifa.