March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWAUWASA yatoa elimu kwa wananchi NaneNane

*Yaombwa kupanua wigo mfumo wa maji taka 

*MWAUWASA yasisitiza ulipaji ankra za maji

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA), katika maonesho ya Wakulima Nane Nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanafanyika Nyamh’onglo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wamefurahishwa na  elimu iliyotolewa na mamlaka hiyo ikiwemo ya mfumo wa maji taka.

Huku wakiiomba MWAUWASA kupanua wigo wa huduma wa mfumo wa maji taka katika maeneo mengi zaidi ili kuondokana na utiririshaji wa maji hayo ovyo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa MWAUWASA Jonas Christopher aliyekaa,akitoa elimu kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda la mamlaka hiyo katika maonesho ya Wakulima Nane Nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanafanyika Nyamh’onglo wilayani Ilemela mkoani Mwanza

Akizungumza mara baada ya  kutembelea banda la MWAUWASA,mmoja wa wananchi hao, Bryton Chacha, amesema,kutokana na elimu alioipata ameweza kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo, ikiwemo ya uondoshwaji maji taka kwa njia ya mfumo.

“Nimeweza kujifunza na kuona,mfumo wa uondoaji maji taka ambao hauhitaji mtu kuchimba shimo kwa ajili ya sinki,bali MWAUWASA wanakuunganishia huduma kwa urahisi,hali inayosaidia kubana matumizi ya ardhi na kuepuka kutiririsha maji taka hasa maeneo ya milimani,”.

Lameck Abel,ameiomba MWAUWASA kufikisha huduma hiyo ya mfumo wa maji taka maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza ili kuondoa changamoto ya wananchi kutiririsha maji taka hasa mvua zinaponyesha na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Kwa upande wake,Kokusima Mugisha, ameeleza kuwa kupitia banda hilo,ameweza kufahamu namna maji yanavyopimwa ubora wa matumizi kabla ya kuwafikia wananchi pamoja na kutambua umuhimu wa kutoa taarifa endapo kutatokea mabomba kupasuka ili kudhibiti upotevu wa maji.

Wakitoa elimu kwa nyakati tofauti  katika maonesho hayo baadhi ya watumishi wa MWAUWASA akiwemo Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka hiyo Jonas Christopher,amesema wameshiriki katika maonesho kwa ajili ya kutoa elimu ya huduma ya maji safi na usafi wa mazingira pamoja na Sheria ya maji.

Jonas amewasisitiza wateja anapopata huduma ya maji safi kuwa  wepesi kulipia ankara ya maji ya kila mwezi,kwani huduma hiyo ni  nyeti na ikizingatiwa maji ni uhai.

“Maji yanapomfikia mteja anawajibu wa kuyalipia  ili huduma iwe endelevu, kwani MWAUWASA inatumia gharama kubwa kufikisha huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo makazi ya watu,bila kuchangia huduma hii ni wazi mamlaka itashindwa kukidhi mahitaji kwa wakati,” amesema Jonas.

Mtaalamu wa Mfumo wa Majitaka kutoka MWAUWASA,Shaban Itegetela,amewaelimisha wananchi namna mfumo wa maji taka unavyofanya kazi huku akisisitiza kuwa mfumo huo kwa sasa upo maeneo ya katika ya  mji lakini katika maeneo ya nje ya mji upo mbio kufika.

Ofisa Mauzo Msaidizi kutoka MWAUWASA, Emmanuel Alex,ambaye ametoa elimu juu ya usomaji wa dira za maji,ameihimiza umuhimu wa wananchi au mteja kushiriki katika usomaji wa dira za maji ili kuepuka kubambikiwa ankra za maji.

Mtaalamu wa Mfumo wa Majitaka kutoka MWAUWASA,Shaban Itegetela,akimuelekeza mmoja wa wananchi namna mfumo wa maji taka unavyofanya kazi
Ofisa Mauzo Msaidizi kutoka MWAUWASA, Emmanuel Alex,akimuelekeza mmoja wa wananchi waliotembelea banda lao kwenye maonesho ya Wakulima Nane Nane namna kusomaji wa dira za maji