December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWAUWASA yapokea mabomba kwa ajili ya mtandao wa maji Kilomita 24

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imepokea shehena ya mabomba yenye gharama ya bilioni 2.4 kwa ajili ya kulazwa kwenye mtandao wa maji wa Kilomita 24 maeneo ya Buswelu, Nyamadoke na Kahama wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya shehena hiyo ya mabomba Septemba 12, 2023, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya amesema mamlaka hiyo inatekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo inayohudumia.

Hiyo yote ni katika kuhakikisha inaimarisha huduma ya maji jijini hapa na kuwapunguzia adha wananchi sambamba na kufikia adhima ya Serikali ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

“Hii ni shehena ya kwanza na tunatarajia siku mbili zijazo tutapokea shehena nyingine kwa ajili ya maeneo ya Luchelele, Ilalila na Kisesa,” amesema Neli.

Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa jitihada zake za makusudi za kuimarisha hupatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza.

“Septemba 15, 2023 MWAUWASA tunaanza majaribio ya awali ya mradi wa Butimba hivyo tutakuwa na ongezeko la maji kutoka Butimba kadri mradi unavyoendelea kukamilika,” amesema Neli.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Buswelu, Sarah Ng’hwani ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma ya maji jijini Mwanza huku aki
wasihi wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji.

“Tunawasihi wananchi watambue kwamba miradi hii imeletwa na Serikali kwa gharama kubwa kwa ajili yao hivyo wanakila sababu ya kuhakikisha inatunzwa,” amesisitiza.