Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Neli Msuya ameeleza umuhimu wa Mamlaka za Maji za maeneo jirani kushirikiana katika kuwatatulia wananchi kero ya maji.
Amesema hayo wakati wa kikao chake na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi Kigoma (KUWASA), Poas Kilangi Oktoba 21, 2023 kilichohudhuriwa na Menejimenti ya MWAUWASA ambapo kwa pamoja wakurugenzi hao wameahidi kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kusaidiana kila inapobidi ili dhamira na lengo la kumtua mama ndoo ya maji kichwani itimie.
Amesema suala la ushirikiano miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji limekuwa likielekezwa kila mara na Waziri wa Wizara hiyo Jumaa Aweso kwa nyakati tofauti tofauti.
“Waziri alikwishatoa maelekezo kuhusu kuimarisha ushirikiano miongoni mwa taasisi zinazoshughulika na masuala ya maji,sasa ni wakati tutazame maeneo ya ushirikiano kwa manufaa ya wananchi tunaowahudumia,” amesema Neli.
Neli amesema kwa sasa MWAUWASA inashirikiana kwa karibu na Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) katika kuhakikisha huduma ya maji kwenye maeneo inayohudumia inaimarika na kuwaondolea adha wananchi.
“Itakua ni vizuri zaidi tukatoka nje ya maeneo yetu katika kushirikiana hii litasaidia kutimiza adhima ya Serikali ya kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi,ninaamini kuna jambo ambalo KUWASA inaweza kutusaidia na vilevile hatuwezi kukosa jambo la kuisaidia na nyingi katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KUWASA Poas Kilangi amesema jambo la ushirikiano halikwepeki na ameahidi kushirikiana na MWAUWASA pamoja na mamlaka zingine za maji katika nyanja mbalimbali ili kutimiza dhamira ya serikali ya kuwafikishia huduma ya maji Watanzania.
“Sote lengo letu ni moja ambalo ni kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi, hatuna sababu ya kufanya kazi kwa kujifungia, nina ahidi tutashirikiana kwa karibu na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazotukabili ili tuimarishe hali ya huduma,” amesema.
Katika kikao hicho,Kilangi ameiaga Menejimenti ya MWAUWASA kwani tangu ateuliwe na Waziri wa Maji Juni 22, 2023 hakupata fursa ya kuagana.
Kabla ya kuwa Mkurugenzi wa KUWASA Kilangi alikuwa mtumishi wa MWAUWASA kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Ununuzi.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango