Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Majaji kutoka nchini Ghana na Nigeria ulioko nchini kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu Sheria.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekutana na ujumbe huo tarehe 2 Juni, 2025 katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukutana na Ujumbe huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ujumbe huo umekuja nchini kufanya ziara ya mafunzo kuhusiana na masuala ya kisheria hususani kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Tumepokea ugeni kutoka nchini Ghana ambao unaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Ghana ameambatana na timu yake pamoja na majaji kutoka Nigeria ambao wamekuja kujifunza juu ya masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa ujumbe huo umeambatana na Taasisi ya GIZ inayosimamia mradi wa kuchapisha sheria, maamuzi pamoja na kanuni mtandaoni ujulikanao kama TanzLII, ambapo aliishukuru taasisi hiyo kwa kutekeleza mradi huo na amewaahidi kuendelea kuuhudumia mfumo mara baada ya mradi huo wa TanzLII kukamilika.

“Tunawashukuru sana GIZ kwa kuhakikisha kwamba sheria zetu tunaziweka kwenye mfumo wa TanzLII hivyo kurahisisha katika utoaji wa huduma mbalimbali za kisheria, na sisi tunawaahidi kuendelea kuutumia mfumo.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Kwa upande wake, Jaji Jennifer Dadzie kutoka Mahakama ya Rufani nchini Ghana, ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapokezi mazuri waliyoyapata na ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwakua wameweza kujifunza namna Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inavyotekeleza majukumu yake.

“Lengo la ziara hii ni kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisheria yanavyoendeshwa hapa Tanzania, tumetembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tumeweza kujifunza na kuona Ofisi hii inavyotekeleza majukumu yake.” Amesema Jaji Dadzie.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge awataka RUWASA kukamilisha mradi wa maji kwa wakati Kilindi
Balozi Nchimbi aongoza waombolezaji kumuaga Mzee Mongella
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mama yake mzazi