Na Thomasi Kiani, Ikungi – Singida
MWANAMKE mmoja mkazi wa Kitongoji cha Munkhonje, Kijiji cha Mtunduru, Kata ya Mtunduru, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Asha Rajabu (40) ameuawa na mwili wake kutupwa shambani ukiwa hauna nguo.
Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na kamanda wa Polisi Mkoani Singida kamishina msaidizi wa polisi ACP Sweatbert Njewike zinasema uchunguzi wa Polisi umebaini mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha kichwani, shingoni na miguuni na alikatwa na kitu chenye ncha kali.
ACP Njewike amesema mwili wa marehemu Asha Rajabu ulikutwa shambani mita 100 kutoka kwake tukio ambalo lilitokea usiku wa jumapili iliopita baada ya kuondoka kwenye baa ya kunywa pombe za kienyeji wakiwa na Saidi Ramadhani ambae alikuwa naye.
Kamanda Njewike amesema mwili wa marehemu uligunduliwa kesho yake asubuhi na watu wa eneo hilo na kutoa taarifa Ofisi ya Kijiji na Kata baadae Polisi Ikungi, na mwili wake ulikutwa hauna nguo kuashiria kuwa muuaji alimvua nguo zote marehemu Asha na kuuacha mwili huo hauna nguo.
Kamanda Njewike amesema mmuaji baada ya kutenda kosa hilo alikumbia na mpaka sasa hajaonekana na anatafutwa na polisi hivyo amewataka wananchi kushirikiana na polisi ili Saidi Ramadhani aliyekuwa naye siku ya mwisho akamatwe ili aweze kufikishwa kituoni kusaidia polisi kupata maelezo ya uhakika juu ya tukio hilo.
Uchunguzi wa timu ya waganga kutoka Ikungi umebaini kuwa Marehemu Asha Rajabu alikufa kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kukatwa shingo kichwa na miguu huku mwili huo kuburuzwa hatua kadhaa mbali na njia ndani ya shamba la jirani yake.
Baada ya uchunguzi wa polisi na waganga ndugu waliruhusiwa kuuchukua mwili wa marehemu kwa hatua zote za mazishi na polisi bado wanaendelea na upelelezi wake na kumtafuta mhusika wa tukio hilo la kikatili ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu mashtaka yake.
Na katika tukio jingine Mwenyekiti wa kitongoji cha kaselya Kata ya Kaselya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Haruna Ntandu Kituu amefikishwa kituo cha polisi Iramba – Kiomboi akituhumiwa kumkata kwa panga Mgoni wake baada ya kumkuta akiwa ndani nyumbani kwake akiwa na mke wake mdogo.
Habari zilizotolewa na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaselya Mohamed Mkanga zinasema mara nyingi Mwenyekiti huyo alimuonya Mgoni wake Iboma Muna aache mchezo wake kwa mkewe Lohini lakini hakuacha, na juzi usiku alikutwa akiwa na mke wa Mwenyekiti wakiwa chumbani wakivunja amri ya sita na kukatwa na panga mikono yote.
Mohamed Mkanga amesema baada ya kukatwa mikono alikimbia hadi Zahanati lakini uongozi wa zahanati ulimkatalia matibabu hadi wapate hati ya dharura kutoka Ofisi za Kijiji au Polisi lakini baada ya rai nyingi kutolewa na yeye kusema ukweli yaliomkuta alitibiwa ameshonwa nyuzi 7 mkono wa kushoto na 4 mkono wa kulia na kesi inaendelea.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang