Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Boaz Edimund(22) Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine(SAUT),kampasi ya Mwanza aliyekuwa anasomea Shahada ya kwanza ya Sanaa ya Elimu amefariki mara baada ya kuzama kwenye maji alipo teleza kwenye jiwe wakati akijiandaa kuogelea ndani ya Ziwa Victoria eneo la Sweya Kata ya Luchelele wilayani Nyamagana jijini hapa.
Mwanafunzi huyo ambaye ni Mkazi wa Mbozi mkoani Songwe ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho siku ya Mei Mosi mwaka huu majira ya jioni marehemu akiwa na wanafunzi wenzake ambao ni rafiki zake wawili walikwenda kupiga picha eneo hilo la Sweya ambapo baada ya upigaji wa picha aliamua kuingia ndani ya maji kwa ajili ya kuogelea lakini bahati mbaya aliteleza na kuzama ndani ya maji.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho David Lameck ameeleza kuwa walifika eneo hilo na kuanza kupiga picha kwa ajili ya’location’ na baadae wakaamua kuoga.
“Akavua nguo zake akasimama sehemu ambayo ilikuwa na jiwe akateleza maana lile jiwe lilikuwa limeisha tengeneza mtaro hivyo baada ya kuteleza wale waliokuwa naye hawajui kuogelea hivyo alikosa msaada hatimaye akawa amezama majini na baada ya hapo taarifa zilitoka uongozi wa mtaa ulifika mapema , serikali ya wanafunzi SAUT na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndipo uokoaji iliposhindikana kwa sababu ilikuwa giza na maji yalikuwa machafu na kiwango kikubwa cha maji ambacho kimeongezeka,”ameeleza Lameck.
Kwa upande wake Mlezi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine(SAUT) Father Japhet Njaule, ameeleza kuwa ni kawaida ya wanafunzi kuzunguka ziwani hapo kwa minajili ya kupiga picha tu lakini waliamua kuogelea na walikuwa watatu katika msukosuko huo marehemu aliteleza na kupotea ndani ya ziwa ambapo wenzake pamoja na watu wengine wakiwemo wavuvi waliokuwa pembeni walifanya jitihada za kumtoa lakini ikashindikana.
“Taarifa zikafika chuoni jitihada zikafanyika, Mimi nilikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio na tukatoka taarifa kwa polisi na baadae Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakafika kwa sababu majira yalikuwa yamesogea jioni saa 12.30 kuelekea giza walijaribu kumtafuta lakini ikashindikana hivyo wakaamua kwamba kesho yake wangeweza kuja na kuanza tena zoezi bahati nzuri leo wamefika asubuhi mapema 12.30 na tumempata kijana wetu ambaye ameisha fariki,”ameeleza.
Ametoa rai kwa wanafunzi ambao ni wageni hasa wale wa mwaka wa kwanza wawe makini na maeneo hayo hata hivyo chuo hicho kimekuwa kikitoa elimu kwa wanafunzi ili waweze kuelewa mazingira hayo.
“Mara nyingi sehemu kubwa ambazo tumekuwa tukielezea ni sehemu za kingo za ziwa Victoria kwamba ni maeneo hatarishi sababu wengine wanakuja hawajui kuogelea pia ni maeneo ambayo kuna mamba na nyoka na kadhalika hivyo chochote kinaweza kutokea ingawa wakati mwingine wanajisahau kwa sababu ya ujana wanajikuta wanatumbukia humo alafu matukio kama haya yanatokea,”.
Akizungumzia tukio hilo Mei 2,2024 mbele ya Waandishi wa Habari mkoani hapa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza Kamila Labani, ameeleza kuwa majira ya saa mbili usiku,Mei Mosi mwaka huu jeshi hilo lilipokea taarifa ya kuzama maji kwa mwanafunzi huyo baada ya zoezi la upigaji wa picha aliamua kuingia ndani ya maji kwa ajili ya kuogelea.
“Eneo waliokuwa wanapiga picha lina miamba ambayo imeingia mpaka ndani ya maji, alisimama juu ya mwamba mmoja na akaingia ndani ya maji kuogelea bila kujua kuwa maji yale yana kina kirefu ambapo hakufanikiwa kutoka baada ya kuingia hivyo akawa amezama ndani ya maji bila kuogelea,rafiki zake walitoa taarifa majira ya saa mbili usiku na Askari wetu wa majini wazamiaji walikwenda eneo la tukio,”ameeleza Kamila na kuongeza kuwa
“Kutokana na giza Askari hao hawakuweza kuendelea na zoezi la utafutaji hivyo ikawalazimu leo Mei 2,2024 walirudi eneo la tukio ambapo zoezi hilo lilianza majira ya saa kumi na mbili asubuhi na baada ya jitihada zilizofanywa na Askari hao waliweza kuopoa mwili wa Boaz ambaye alikuwa amezama na kuingia kwenye mapango yaliopo ndani ya maji,”.
Hata hiyo Kamila ameeleza kuwa mwili wa marehemu huyo baada ya kufanikiwa kuopolewa wameukabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya taratibu nyingine za kijinai ili wao waweze kuendelea nazo.
Sanjari na hayo ametoa rai kwa watumiaji wote wa Ziwa Victoria na wengine wanatumia vyanzo vya maji kama mabwawa maalum ya kuogelea kwa jina la ‘Swimming pool’ na maeneo mengine yote kuwa makini .
“Tunaotumia Ziwa Victoria tunatakiwa kuwa makini zaidi kwa sababu kuna maeneo mengine yana miamba mengine yana mapango hasa kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu mkoani Mwanza t wasiende kuogelea kwenye maeneo tusiyoyafahamu kwanza hatuna vifaa vya uogeleaji na vya usalama lakini taifa linatuhitaji,familia zetu zinatutegemea na jamii zetu tunapotoka zinatusubilia turudi kwa ajili ya kuzitumikia hivyo tuwe makini katika jambo hili,”.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa