Na Esther Macha,Timesmajira Online, Rungwe
MWANAFUNZI wa shule ya msingi Katumba -11 iliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya aitwaye , Bestina Haule ambaye ni mlemavu wa viungo anayetumia miguu kuandika amemuomba Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kumsaidia katika masomo yake ili aweze kufikia ndoto ya masomo yake kuwa Daktari.
Mtoto Haule alifika katika shule hiyo akitokea mkoani Ruvuma mwaka ,2020 kutokana na kushindwa kuendelea na masomo katika shule aliyokuwa akisoma hivyo kuhamishiwa katika shule ya msingi mchanganyiko ya Katumba -11 iliyopo mkoani Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari Mtoto Bestina amesema kuwa Mungu amsaidie aweze kufika mbali zaidi kwani anatamani kuwa daktari .
Mkuu wa kitengo cha watoto wenye ulemavu Shuleni hapo , Mwl, Bonifasi Jakob amesema kuwa Mwanafunzi huyo baada ya kufika shuleni hapo walimwangalia kama kuna uwezekano wa kumfanyia oparesheni ya mikono ili aweze kusoma na kuandika lakini ilishindikana baada ya wataalamu kushauri kuwa itakuwa ngumu kumfanyia oparesheni ya mikono.
Mwl.Jakob amesema baada ya kuona hakuna uwezekano wa kufanyiwa oparesheni waliamua kuchukua jukumu la kuanza kumpa mazoezi ya kumfundisha kuandika kwa kutumia miguu yake.
Amesema kwa sasa Mtoto huyo anaandika vizuri akiwa na maendeleo mazuri darasani ambapo kati ya wanafunzi 85 amekuwa akishika nafasi ya tisa hadi ya 16 licha kuwa na changamoto ya ulemavu.
Job Mwangungulu ni mwalimu Mkuu msaidizi shule ya msingi Katumba-II iliyopo wilayani Rungwe mkoani mbeya anasema kuwa mtoto Bestina amekuwa akitumia miguu katika kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufua,kula kwa kutumia kijiko na shughuli nyinginezo.
Mtoto mwingine mwenye ulemavu wa viungo , Malisoro Aloyce, mkazi wa Lupa wilayani Chunya ,anasema kuwa alikimbia manyanyaso kutoka Shule ya msingi Lupa tinga tinga baada ya kupata manyanyaso pamoja na kutengwa na watoto wenzake amesema kuwa alikuwa anaonewa na watoto wenzake
Amesimulia mkasa mmoja uliowahi kumkumba baada ya kuitwa mwalimu wake akiwa golini akidaka mpira akiwa na mzazi wake kwamba kuna shule nzuri ya Katumba –II na ndipo alihamishiwa shuleni hapo.
Amesema alifurahishwa na kuridhishwa kufika shuleni hapo baada ya kukuta umoja na ushirikiano mkubwa baina ya wanafunzi kwa na walimu na anamshukuru Mungu kwa kuendelea kufundishwa vizuri hadi wanaelewa.
Hata hivyo mtoto huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha ndani na badala yake wawapeleke shuleni hapo ambapo kwa upande wake anatamani kuwa Mwanajeshi mara baada ya kuhitimu.
Shule hiyo licha kutoa elimu bora kwa watoto wenye ulemavu imekuwa ikikab iliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo uchakavu wa baadhi ya madarasa,upungufu wa viti kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo ,pamoja na madawati .
Changamoto hizo zimekuwa zikitatuliwa na serikali pamoja na taasisi mbali mbali ikiwemo Taasisi ya Tulia Trust ambao wamekuwa wakiwawezesha watoto mahitaji mbali mbali ikiwemo viti mwendo kwa wenye ulemavu .
Meneja wa Tulia Trust Jackline Boaz amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbali mbali katika shule hiyo ili kuweza kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu katika mahitaji mbali mbali.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best