June 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanafunzi MUST mbaroni kwa  tuhuma za mauaji

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) mwaka wa kwanza aitwaye Emilian Duzu (21) anashikiliwa na Jeshi la  polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya Mwanafunzi mwenzake wa Chuo hicho mwaka wa tatu aitwaye Gerald  Said (22).

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea Juni 14, 2025,majira ya saa 11:00 Alfajiri katika Klabu iitwayo Mbeya Pazuri iliyopo Jijini Mbeya .

Aidha Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa mtuhumiwa Duzu alimjeruhi Said  ambaye kwa sasa ni marehemu kwa kumchoma kitu chenye ncha kali tumboni hali iliyopelekea kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu lakini ilipofika saa 7:00 mchana  Said alifariki dunia.

Kuzaga amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na ulevi wa kupindukia wakiwa eneo la ndani la klabu hiyo ambapo walinzi (Mabaunsa) waliwaamua na ndipo mtuhumiwa alitoka nje na kuelekea eneo la maegesho.

Hata hivyo amesema kuwa alipokuwa kwenye eneo ambalo alikuwa ameegesha gari ndipo GSaid ambaye kwa sasa ni marehemu alimfuata kwa lengo la kuendelea kugombana ndipo mtuhumiwa alimchoma kwa kitu chenye ncha kali.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani havina nafasi katika jamii na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo makini na halitasita kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa Wanafunzi kuzingatia masomo na kujiepusha na vitendo visivyofaa ikiwemo ulevi wa kupindukia kwani ni hatari kwa afya zao na maisha yao.