*Inadaiwa tukio hilo lilitokea wakati wakicheza mchezo wa kuchapana na fimbo
Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi
Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Mtenga wilayani Nkasi mkoani humo Samwel Kayoka (16),kwa tuhuma za mauaji ya mdogo wake Jackson Kayoka (14) kwa fimbo walipokuwa wakicheza mchezo wa kuchapana kwa fimbo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa,SACP.Shadrack Masija ni kuwa tukio hilo limetokea jana, majira ya saa sita mchana katika kijiji cha Mtenga “A”,wakati watoto hao walipokuwa wakicheza kwa kuchapana na fimbo,inadaiwa katika mchezo huo marehemu alipigwa na fimbo kichwani na kudondoka chini.
Amesema kuwa baada ya marehemu kuanguka chini na kupoteza fahamu alichukuliwa na kukimbizwa katika zahanati ya Mtenga na wakati jitihada za kumpatia matibabu zikiendelea alipoteza maisha.
Masija alidai kuwa kwa sasa wanaendelea kumshikilia mtoto huyo huku wakiendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kuwa baada ya hapo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Awali Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Romwald Kapele, alidai kuwa watoto hao ni wa familia moja,na kuwa katika mila za kabila la wasukuma ni kawaida kwa watoto wa umri huo kucheza michezo ya namna hiyo ya kupigana kwa fimbo na kuwa hata baada ya tukio hilo kutokea mtoto anayetuhumiwa hakukimbia na badala yake alikua akishangaa tukio lenyewe.
Alidai kuwa baada ya taratibu mbalimbali za Kipolisi kufanyika ndugu walikabidhiwa mwili wa marehemu na taratibu za mazishi zimefanyika jana.

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI