Na Esther Macha,TimesMajira Online,Mbeya
MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Uhamila wilayani Mbarali mkoani Mbeya,Gilison Ngungulu (8)amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa Kanisa la GMCL.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya,Ulrich Matei amewaeleza waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo limetokea Desemba 14, mwaka huu majira ya saa 19.00 usiku katika mtaa wa wa Isisi uliopo Tarafa ya Rujewa.
Matei amesema kuwa, chanzo cha tukio hilo ni kunyesha kwa mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ambayo ilipelekea ukuta wa jengo la kanisa kuanguka wakati mtoto huyo akicheza eneo hilo na watoto wenzake ambao hawakupata madhara yoyote katika tukio hilo.
Akielezea zaidi Matei amesema kuwa, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali na kukabidhiwa kwa ndugu.
Kamanda Matei ametoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kuchukua tahadhari kwa watoto wao hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinaedelea kunyesha katika maeneo mbalimbali kwa kuhakikisha hawachezi maeneo hatarishi.
“Ndugu wazazi angalieni watoto wenu kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha katika maeneo yote hatarishi ili wasiweze kupata madhara,”amesema Matei.
Hata hivyo Kamanda Matei amesema kuwa, ni wajibu wa kila mzazi na jamii kuhakikisa wanafunika visima vya maji vilivyo wazi,mashimo, kwani ni hatari endapo yatajaa maji.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi