Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Muheza
MGOMBEA ubunge jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma (Mwana FA) ameahidi kuineemesha na kuendeleza zaidi sekta ya michezo.
Mwana FA ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za jimbo hilo zilizoshirikisha viongozi mbalimbali na wasanii kama sehemu ya kumuunga mkono.
Amesema, atahakikisha katika kipindi cha miaka mitatu ya anafanikisha jambo hilo kwa kuufanyia maboresho makubwa Uwanja wa Jitegemee ambao hutumika kwa mechi mbalimbali ikiwemo ikiwemo pia mapambano ya ngumi.
Pia amesema, wataweka mikakati madhubuti ambayo itaiwezesha timu ya Muheza united inafanya vizuri na kufanikiwa kupanda madaraja mbalimbali hadi kufikia Ligi Kuu pamoja na kuandaa mashindano mbalimbali ambayo yataibua hamasa ya michezo na kukuza vipaji.
Mbali na ahadi hiyo kiongozi huyo pia amesema, atahakikisha yeye ni kitabu kipya chenye mawazo tofauti na yupo tayari kuwatumikia wana-Muheza kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.
Mwana FA amesema, atahakikisha anazisema changamoto zote za wanamuheza katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwaomba wananchi kutoa kura za kutosha kwa CCM.
”Nitahakikisha natumia miaka mitatu kuukarabati uwanjwa wa Jitegemee ambao tunaimani itatoa hamasa kubwa ya michezo ambayo kwa sasa ni miongoni mwa sekta inayotoa ajira kwa vijana wengi. Pia nitawatumikia wananchi tutajitahidi kuhakikisha tunakuwa na Muheza mpya yenye maendeleo,”amesisitiza Mwana na kuongeza.
“Yupo tayari kuendeleza mradi wa maji ulioanzishwa na mbunge aliyepita Balozi Adadi Rajab, kutatua kero ya barabara Amani ili itengenezwe kwa kiwango cha lami na kuchochea maendelea=o zaidi katika jimbo hilo”.
Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo balozi Adadi Rajabu ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika michezo, amewataka wanamuheza kuondoa makundi na kuhakikisha wanampa Mwana FA ushindi wa kishindo.
Amesema, atahakikisha anampa ushirikiano wa kutosha kumuongoza katika kufanikisha vipaumbele vyake ikiwemo kwenye kukuza vipaji kwani kwa miaka mingi amekuwa akiendesha michuano ya Soka ‘Adadi Cup’ kwa ajili ya kuwasaidia vijana lakini pamoja na kumfahamisha miradi yote aliyoianzisha anaiendeleza kwa maslahi ya Muheza.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu amewataka wakazi wa Tanga kuacha kuyumbishwa na vyama vingine na kuwataka kusimama imara kwajili ya maendeleo ya nchi kwani mambo mengi muhimu yamefanyika nchini.
”Wananchi msiyumbishwe na hao wanaochanganya picha mkadanganywa na ule umati mnaouona zile ni picha wanachanganya wanachokifanya ni ujanja wa kulaghai na utatufikisha pabaya,”amesema Shekifu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema wanamuheza wanabahati kupata kijana mahiri na mnyenyekevu ili ayaendeleze yale aliyoyafanya balozi Adadi Rajab.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM