Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KAIMU kocha mkuu wa klabu ya Yanga Juma Mwambusi ameweka wazi kuwa kwa sasa kikosi chake kimeanza kuimarika na kurudi kwenye makali yake hivyo anaamini mambo mazuri zaidi yanakuja kutokana na kucheza mpira wenye malengo.
Kocha Mwambusi ametoa kauli hiyo baada ya juzi kupata ushindi wa goli 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani dhidi ya Biashara United goli pekee kilifungwa dakika ya 58 na mshambuliaji Yacouba Sogne.
Katika mchezo huo Yanga walifanikiwa kumiliki mchezo kwa asilimia 59 kwa 41 za wapinzani wao, wakipiga mashuti 12 sita yakilenga lango wakati Biashara walipiga masuti matatu na moja ndilo lililolenga lango.
Ushindi huo ni wa pili msimu huu kwa Yanga ambao walifanikiwa kuwafunga Biashara goli 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani wa Kumbukumbu ya Karume Mara katika mchezo uliochezwa Oktoba 31, 2020 na kufanikiwa kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakifikisha alama 54.
Ameisema, kiwango walichokionesha Yanga katika mchezo huo kimeanza kwenda katika kile anachokitaka hivyo anaamini ikiwa wataweka juhudi zaidi katika mazoezi yao kuelekea mechi zijazo basi watarudi haraka katika makali yao kwani wameanza kucheza mpira wenye malengo.
Mwambusi amesema kuwa, kama wangekuwa makini katika mchezo dhidi ya Biashara basi walikuwa na uwezo wa kupata ushindi wa zaidi ya goli 1 lakini ubora wa wachezaji wa wapinzani wao uliwafanya wachezaji kupoteza umakini na kushindwa kutumia nafasi nyingi walizozitengeneza.
“Wenetu walicheza kwa kulinda sana na ndio maana walikuwa wakijaa mbele ya lango lao lakini tulijitahidi kucheza kwa mapana lakini hawakutupa nafasi katika kipindi cha kwanza jambo lililofanya pia kupoteza umakini. Lakini mapumkiko tulipeana maelekezo na kutaka kutumia dakika 15 za kwanza kupata goli.”.
“Japokuwa tulitengeneza nafasi chache lakini moja tuliyoitumia imetupa alama tatu na kikubwa kwangu kama mwalimu ni kuiona Yanga inaanza kuja katika kiwango ninachokihitaji na kucheza mpira wenye malengo,” amesema Mwambusi.
Kocha huyo ameweka wazi kuwa kwa sasa wanatakiwa kuweka mkazo zaidi kwenye upande wa umaliziaji kwani bado wachezaji wake wana uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za mabao lakini bado wanashindwa kupata goli nyingi.
“Hatuwezi kuchoka na hatukati tamaa bali tutaendelea kufanya marekebisho zaidi katika eneo la umaliziaji ili kupata magoli mengi zaidi katika mechi zetu zijazo ambazo wanahitaji kushinda ili kuendelea kuongoza ligi na kutwaa ubingwa wa msimu huu,”.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM