November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwambe ataka CTI kuitumia TNBC kutatua changamoto

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Bw.Geoffrey Mwambe ameitaka jamii, jumiya ya wafanyabiashara nchini inapoandaa vikao vyake na Wizara mbalimbali ni vyema vikafanyika chini ya uratibu na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ili kuleta wepesi wa ufuatiliaji wa changamoto na mapendekezo kufika katika ngazi, husika jambo litakalo boresha mazingiraa ya biashara nchini.

Waziri Mwambe alizungumza hayo wakati akifungua mkutano wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) uliolenga kujadili changamoto za zinazoikabili sekta ya viwanda nchini na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

“Ni muhimu mikutano kama hii ishirikishe TNBC ili tija iweze kupatikana ya kuandaa mikutano kwani mapendekezo na changamoto zitakazotolewa vitawasilishwa katika kila wizara kwa umuhimu wake na kutafutiwa ufumbuzi,” amesema Waziri Mwambe.

Ameongezea kuwa inaposhirikishwa TNBC inakuwa ni kiunganishi kati ya sekta binafsi na Serikali, kwani jukumu lake kubwa ni kusimamisha majadiliano na kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia uwekezaji nchini.

Baadhi ya Wajumbe wakifatilia mada kwenye mkutano wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania(CTI) uliofanyika jijini Dar es Salaam mwisho mwa wiki kujadili changamoto za zinazoikabili sekta ya viwanda nchini na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

“Mbali na kuishirikisha TNBC ambacho ndicho chombo kinachosikiliza changamoto zenu, nakubaliana na ombi mlilotoa la kutaka kila mwekezaji kwenye kiwanda asajiliwe na CTI ili kufanya urahisi wa ufatiliaji wa changamoto zenu kupitia mikutano ya majadaliano,” ameeleza.

Katika kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa bora zaidi, Serikali imejipanga kufanya mabadiliko ya sheria na sera mchakato ambao upo tayari na muda sio mrefu utawasilishwa bungeni kwa majadiliano.

“Serikali imekusudia kufanya mapitio upya ya sheria na sera ya uwekezaji ili kwenda sambamba na mazingira ya sasa jambo ambalo litaongeza kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwa kuyaangalia maeneo ambayo yamekuwa changamoto kubwa hapa nchini,’’ amesema Waziri Mwambe

Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara kuwa waaminifu na kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kuendelea na ujenzi wa miundombinu ikiwemo vituo vya afya, reli, barabara, viwanja vya ndege pamoja na ujenzi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga alisema muundo mpya wa Baraza umelenga kufanya vikao kuanzia ngazi ya wilaya na mkoa ili kupata ufumbuzi wa changamoto za ufanyaji biashara na uwekezaji.

“Mabadiliko haya ya kimuundo ya Baraza yamelenga kuleta mazingira rafiki ya ufanyaji biashara na uwekezaji hasa ukizingatia Tanzania imekuwa na faida ya kuwa na rasilimali za kutosha, amani na utulivu wa kisiasa,’’ amesema Dkt. Wanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Uwekezaji) Bw.Geoffrey Mwambe(kushoto) akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania(CTI) uliofanyika jijini Dar es Salaam mwisho mwa wiki kujadili changamoto za zinazoikabili sekta ya viwanda nchini na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) Dkt.Godwill Wanga, wapili kulia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CTI,Dkt.Samuel Nyantahe na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa CTI, Bw.Paul Makanza.

Dkt. Wanga aliwahakikishia CTI kuwa Baraza litaendelea kufanya majadiliano na sekta binafsi kwa kuwa ndicho chombo maalum kinachounganisha serikali na sekta binafsi.

“Baraza limekuwa kiunganishi muhimu kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuangazia changamoto za ufanyaji biashara na uwekezaji, hivyo tuitaendelea kufanya majadiliano na wadau wa sekta binafsi ili kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikirudisha nyuma ukuaji wa biashara na uwekezaji,’’ amesema

Naye Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza alisema kumekuwa na mwelekeo mzuri wa kushughulikia changamoto za wenye viwanda, lakini ipo haja ya kuongeza mikakati madhubuti zaidi ya kuendeleza na kuipa ushindani sekta ya viwanda ili kwenda sambamba na maono ya Serikali.

“Viwanda kama zilivyo sekta zingine, kumekuwa na changamoto nyingi na zipo ambazo zimepatiwa majibu baada ya vikao kadhaa vya majadiliano. Mapendekezo yetu kwa sasa ni kuona mikakati mingi zaidi na shirikishi inawekwa ili kuongeza machango wa sekta hii kwenye ukuaji wa pato la taifa na ajira kwa vijana,’’ amesema Makanza