Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Mbeya
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, amewataka viongozi wa Chama hicho hususani Wenyeviti wa Mitaa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo katika maeneo yao.
Amesema, uongozi walionao umetokana na imani ya wananchi kwa kuwachagua, ili waweze kuwawaikilisha vyema katika Serikali kuu na kuwaletea maendeleo katika maeneo yao pamoja na kuwatatulia changamoto zao.
Akizungumza na Wenyeviti wa Mtaa, Makatibu Kata na Madiwani Jijini Mbeya Desemba 17, 2024, Mwalunenge amesema ni vyema kila mmoja akatambua wajibu wake katika kuwatumikia wananchi bila kuangalia hali walizonazo.
“Mkawatumikie watu bila kubagua na bila kuchagua huyu ana uwezo au hana uwezo, nikigundua hayo yanafanyika unanyanyasa watu na hutatui changamoto zao, kwa sababu sisi kama chama ndiyo tuliokupa dhamana, hatutasita kukusimamisha na hilo naongea wazi kweupe.
Ombi letu kwenu kama chama ni kwenda kufanya kazi kwa ajili ya wananchi bila kuchoka na bila kujali masaa ya kazi ili wananchi waone kupanga kwao foleni na kukupigia kura kuna thamani”, amesema Mwalunenga.
Pia ameendelea kuwasisitizia viongozi hao kutambua umuhimu wa Serikalia ya Mtaa, kuwa ndiyo msingi wa Serikali kuu na kuwataka Wenyeviti wa Serikali ya Mtaa kufanya kazi yao kwa weledi, ili kuwapa wananchi matumaini na kuendelea kukiamini CCM na Serikali yake.
“Serikali ya Mtaa ndiyo msingi wa Serikali kuu, Miradi yote inayotekelezwa kwenye mitaa yetu Mwenyekiti wa Mtaa ndiye anayejua eneo la kufanyika kwa mradi huo na ni jukumu lake kuufuatilia ngazi kwa ngazi hadi ukamilikaji wake, iwe ni stendi soko au miradi mingine mbalimbali”, amesema Mwalunenga.
Aidha,Mwenyekiti huyo amewataka viongozi hao wa chama kuwa na mahusiano mazuri, hali itayopelekea kuwepo na ufanisi mzuri katika majuku yao ya kazi na si magonvi yanayotokea kwa baadhi yao.
Amesema “Mwenyekiti wa Mtaa na Katibu wa Chama kwenye Kata na viongozi wengine ni lazima muongee lugha moja..lakini unakuta Katibu wa Chama kwenye Kata na Mwenyekiti wa Mtaa hawapatani ni ufitini, majungu, chuki na hila mtasimamiaje miradi? ni lazima muongee lugha moja na tukifanya hivyo tutajikuta tunawatumikia wananchi wetu vizuri “, aliongeza Mwalunenge.
Pia amewaonya Wenyeviti wa Mtaa hao kutokwenda kutumikia watu kwa maslahi yao binafsi na badala yake wawatumikie wananchi wote kwa maslahi ya Taifa.
“Pia jambo lingine msiende kutumikia watu bali mkatumikie wananchi wote kwa ujumla kwa maslahi ya Taifa na Chama kilichowapa dhamana ambacho ni CCM, hapa namaanisha uwenda kuna njia unazozijua wewe mwenyewe zilizokufanya ukapata hiyo nafasi uliyonayo sasa, hivyo si sahihi kwenda kumtumikia yule aliyekufanya umepata nafasi hiyo, kwani wewe umechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mtaa maana yake unakwenda kuwatumikia wananchi wote wa Mtaa huo na si mtu mmoja “, ameongeza Mwalunenge.
More Stories
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa