Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),mkoani Dodoma imemfikisha mahakamani Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Karume iliyopo Kata ya Kibaigwa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kwa kosa la kughushi cheti cha darasa la saba,ili amsaidie mwanafunzi kujiunga na Mafunzo ya kujitolea ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mwalimu mkuu huyo amekuwa akivitoa vyeti hivyo kwa gharama ya sh. 50,000 kwa kila kimoja,ambapo hadi anakamatwa alikutwa ametoa vyeti viwili kwa Mbaraka Juma na Elia Fred wote wakazi wa Kata ya Kibaigwa.
Pia taasisi hiyo imemfikisha katika mahakama ya Wilaya ya Kongwa aliyejifanya mwanafunzi muhitimu wa shule hiyo Mbaraka Juma kwa kosa la kutoa nyaraka za uongo ya kuwa amehitimu darasa la saba katika shule hiyo wakati siyo kweli ili atimize vigezo vya kujiunga na mafunzo ya JKT.
Taarifa kwa vyombo vya habri kwa Mkuu wa Takukuru mkoani Dodoma Sosthenes Kibwengo imesema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kughushi na kutoa nyaraka za uongo ili wafanikishe azma ya kijana Mbaraka kujiunga na JKT.
“Baada ya TAKUKURU kufanya uchunguzi wetu tulibaini mtuhumiwa huyo ambaye ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amekuwa akiuza vyeti hivyo sh.50,000 kwa vijana ili waweze kuvitumia kuomba kushiriki mafunzo ya kujitolea ya JKT.”
“Taasisi yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo ambapo wote walipatiwa dhamani ili kusubiri kutajwa kwa kesi hiyo.”
Aidha TAKUKURU mkoa wa Dodoma imeendelea kuwasisitiza wananchi kutoa taarifa kwa taasisi hiyo pale wanapoona kuna viashiria vya rushwa katika maeneo mbalimbali wanayofanyia shughuli zao.
Kibwengo amesema mapambano ya rushwa ni ya jamii kwa ujumla na si TAKUKURU peke yao ndio maana wamekuwa wakitoa elimu kuhusianana kupambana na rushwa katika maeneo mbalimbali.
Kutokana na hilo amesema wananchi wasisite kutoa taarifa pale anapoona zinaviashiria vya rushwa ili nao waweze kuzifanyia uchunguzi kabla ya kuchukua hatua stahiki za kiutendaji kazi.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili