December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwalimu akanyagwa na tembo hadi kufa

Na Heckton Chuwa,TimesMajira Online,Mwanga

MKAZI mmoja wilayani hapa, Rogers Wilson hivi karibuni amedaiwa kufa baada ya kukanyagwa na tembo katika moja ya kijiji kwenye Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mmoja wa viongozi wa Kata ya Kwakoa wilayani hapa, Rahmu Juma, mkasa huo ulitokea Oktoba 31 mwaka huu saa 2 usiku katika kata hiyo ambapo alisema marehemu, Wilson alikuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kwangu.

“Mkasa huu ulitokea wakati, Wilson alikuwa akirudi nyumbani kutoka dukani alikokwenda kununua bidhaa, ndipo aliposhambuliwa na kundi la tembo ambapo mmoja wa tembo hao alimkanyaga hadi kufa,” alidai na kuongeza kuwa kundi la tembo hao lilitokea Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyoko jirani na eneo hilo.

Akizungumzia mkasa huo Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt.Maurusi Msuha alithibitisha kupata taarifa ya tukio hilo ambapo alisema hatua zilikuwa zinachukuliwa, ili kuhakikisha tembo wanaondoleewa eneo hilo.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kwangu,Agustino Manetho amethibitisha kutokea kwa kifo cha Wilson, ambaye alisema ni mmoja wa walimu wa shule hiyo.

Amesema tembo wanaoshambulia eneo hilo mara kwa mara, wamesababisha hofu miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo.

“Wazazi na walimu sasa tunalazimika kutafuta njia za kuhakikisha ya kuwa wanafunzi wanapata watu wa kuwasindikiza kwenda na kurudi shule, ili kuwaepusha kushambuliwa na tembo wanaozunguka eneo la shule na maeneo mengine ndani ya kata hii,” amesema.