Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online,Dar
KIONGOZI Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, amemualika Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya Kitaifa Vatican kuanzia Februali 11 hadi 12, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema lengo la ziara hii ni kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Vatican.
Alisema Tanzania na Vatican tangu mwaka wa 1960 zimekuwa zikishirikiana katika masuala ya elimu, afya, masuala ya amani na kiroho.
“Kanisa Katoliki linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za chekechea 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110, na vyuo vikuu vitano,” anasema Makamba.
Tofauti za udini hazijawafanya viongozi hawa kushindwa kukaa pamoja na kujadili maslahi ya wananchi na uendelezaji wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Mwaliko wa Papa kwa Rais Samia unatokana na historia ya mahusiano kati ya Vatican na Tanzania hasa katika mchakato wa kutafuta na kudumisha utu, heshima na haki za msingi za binadamu.
Maeneo hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Rais Samia anayoyapa kipaumbele kwenye uongozi wake na mara zote katika uongozi wake amekuwa akisisitiza haki.
Mwaliko wa Papa kwa Rais Samia unatafsiriwa na Watanzania wengi kama neema na baraka kwa nchi yetu, ambayo haina dini, lakini Watanzania wana dini na imani zao.
Mwaliko huo ni mwendelezo wa historia iliyoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Thabit Kombo Jecha, walipotembelea mjini Vatican baada ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, na hivyo kutunukiwa Nishani ya Amani na Mtakatifu Yohane wa XXII.
Baba Mtakatifu Yohane wa XXII alitambua juhudi kubwa zilizofanyika kuunganisha Tanganyika iliyokuwa nchi huru na Zanzibar iliyokuwa imejikwamua kutoka kwenye makucha ya wakoloni kwa Mapinduzi matukufu.
Mtakatifu Yohane XXIII naye aliandika historia kubwa ya mahusiano na Tanzania, kwani ndiye aliyetunga Sala ya Kuiombea Tanzania. Rej. Misale ya Waamini Ukurasa 1510. Hii, ndiyo historia ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican na jinsi ambavyo Mwalimu Nyerere alivyokuwa akifanya shughuli zake kwa ajili ya kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.
“Serikali ya Italia na Vatican wana mahusiano ya pekee sana na Tanzania katika kuleta haki, amani, utu na ubinadamu ,” Anasema Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo.
Uhusiano wa Serikali ya Rais Samia na Vatican unawafurahisha viongozi wa Kanisa Katoliki nchini na hiyo inathibitishwa na kauli ya Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga.
Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alitoa kauli hiyo Mei 17, 2023 kwa niaba ya Maaskofu Katoliki Tanzania ambapo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilipata bahati ya kutembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Hiyo ilikuwa ni fursa kwao kukutana na kusalimiana na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, kusikiliza historia ya mahusiano kati ya Vatican na Tanzania hasa katika mchakato wa kutafuta na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Askofu Nyaisonga anasema, “Maaskofu wamefurahia kuwepo Ubalozini na Hija yetu ya kitume ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni msingi wa wajibu wao kama Maaskofu.
Tumefurahishwa kwa ukarimu na mapokezi makubwa. Lengo likiwa ni kufahamiana na kumpongeza Balozi kwa kazi kubwa anayotekeleza kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Tanzania.
Amemshukuru kwa kuwapitisha Maaskofu kwenye historia kuhusu mchango wa Sheikh Thabit Kombo Jecha, mtu maarufu sana katika harakati za ukombozi wa Zanzibar.
Leo hii kazi hii inaendelezwa na Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Mtoto wa Sheikh Thabit Kombo Jecha, katika mchakato wa ujenzi wa Taifa la Tanzania. Maaskofu wamemwahidi kumweka katika sala na maombi yao, ili aendelee kutekeleza kazi yake vizuri zaidi, ili hatimaye, kumrahishishia Rais Samia kazi zake, ili ziwe nyepesi zaidi na apate hata muda wa mapumziko na kuendelea kuchapa kazi kwa furaha.”
Mbali na kumuombea, Maaskofu pia wanamtakia Rais Samia heri na baraka tele katika majukumu yake ya kuwaongoza Watanzania.
Anaweka wazi kuwa ni furaha kubwa kwa Maaskofu kuona nchi inaendelea, watu wanafurahi na maendeleo yanapatikana na Tanzania kama nchi inazidi kulinda, heshima na tunu zake.
Anasema hayo ndiyo matamanio halali ya Maaskofu Katoliki Tanzania, ndiyo maana wafanyakazi Serikalini wanajituma bila ya kujibakiza ili watanzania wapate furaha, amani na maendeleo.
Askofu Nyaisonga amemwombea Balozi nguvu, ari na moyo wa kutenda yote hayo na kwamba, Maaskofu Katoliki Tanzania wako bega kwa bega kuiendeleza Tanzania.
Mwanadiplomasia, Andrew Jacob, anasema mwaliko huo wa Papa Francis kwa Rais Samia ni heshima kubwa kwa Tanzania hasa kwa kutambua kwamba Vatican ni Jumuiya kubwa yenye mchango mkubwa katika sera na mikakati ya kimataifa na kwamba, mchango wake unathaminiwa sana na Jumuiya ya Kimataifa.
Anasema kikubwa ambacho Vatican inavutiwa na Serikali ya Tanzania ni jinsi inavyounganisha wananchi bila kujali imani zao, ambapo wanafanya shughuli zao kila mmoja kwa imani yake bila usumbufu wowote.
Anasema Serikali inafanya kazi moja ya kuwaudumia wananchi pia na dini zinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi hao hao kiroho, na hiyo ni miongoni mwa siri za mwaliko wa Papa kwa Rais Samia.
“Hakuna haja ya Serikali na dini kugombana wala kukwaruzana kwa sababu wote wanafanya kazi moja kwa wananchi.
Ni bora kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Serikali na dini na nashukuru jambo hili ili kujenga jamii moja yenye familia moja katika kumtukuza Mungu.” Anasema mwanadiplomasia huyo.
Jacob anasema Serikali inatambua juhudi za Kanisa Katoliki katika kuleta maendeleo kwa wananchi hasa ujenzi wa shule na hospitali kama huduma za jamii kwa wananchi pia kutoa huduma za kiroho zinazosaidia kukuza maadili katika jamii.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika