Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Hawa Mwaifunga,amesema Rais Samia Suluhu Hassan,katika kipindi cha miaka 4 tangu aingie madarakani, amesimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kufanyia kazi kero za wananchi.
Mwaifunga, amesema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Manispaa Tabora,katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Ipuli,ambapo amesema mfano wa baadhi ya kero alizowasilisha bungeni na kufanyiwa kazi na Rais Samia,ni uchakavu wa miundombinu ya shule kongwe za msingi katika Maanispaa hiyo ikiwemo ya Town School, Kitete na Isike.

Ametaja mambo mengine yaliyofanywa katika Manispaa hiyo ni kujengwa kwa hospitali mpya ya Wilaya ya Tabora na kuboreshwa kwa miundombinu ya kituo cha afya cha Maili tano.
Miradi mingine ya kimkakati ambayo utekelezaji wake umeanza katika mwaka huu wa fedha ni mradi wa stendi mpya ya mabasi unaojengwa maeneo ya Inala na soko jipya la kisasa linalojengwa katikati ya Mji lilipokuwa soko la zamani.
Amefafanua kuwa kazi ya Mbunge ni kusikiliza kero za wananchi na kuziwasilisha bungeni ili zifanyiwe kazi, jukumu ambalo amedai kuwa amelifanya kwa weledi na kufanikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa kiasi kikubwa.

Amedokeza kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu atagombea Ubunge jimboni humo, bila kutaja atagombea kupitia chama gani, hivyo amewaomba wananchi wamuunge mkono wakati utakapofika ili aendelee kuwatetea bungeni.
More Stories
Mwongozo wa kitaifa kwa watoa huduma za maendeleo ya biashara wazinduliwa
Zanzibar ipo tayari kupokea wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
Elimu ya kilimo tija yawafikia wakulima mikoa mitano.