Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
LICHA ya kukaa kwa muda mrefu mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), kikosi cha timu ya Mwadui FC bado kina matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wao wa leo utakaochezwa saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Mabatini dhidi ya wenyeji Ruvu Shooting.
Mwadui itaingia katika mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutofanya vizuri katika mechi zake nyingi za msimu huu kwani hadi sasa katika mechi 26 walizocheza wameshinda mechi nne, sare nne na kupoteza mechi 18.
Licha ya kushikilia rekodi ya kuwa timu iliyopoteza mechi nyingi msimu huu lakini pia Mwadui imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 47 huku wao wakifunga goli 18.
Pia timu hiyo inasaka ushindi ili kuondoka ana alama zote tatu dhidi ya wenyeji wao ambao waliwalazimisha sare ya goli 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 4 kwenye uwanja wa Mwadui Complex.
Kocha mkuu wa Mwadui FC, Salhina Mjengwa amesema kuwa, hasira waliyonayo baada ya kutofanya vizuri katika mechi zao nane zilizopita ndiyo itakayowafanya kuzindukia katika mchezo wa leo na kuchukua alama zote tatu.
Amesema kuwa, wanatambua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini morali na nidhamu waliyoingia nayo katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Simba ndiyo watakayoingia nayo katika mchezo huo ili kusaidia kufanikisha mkakati wao.
Kocha huyo amesema kuwa, hadi sasa wameshawasoma sana wapinzani wao na watahakikisha wanaingia uwanjani kupambania ushindi ambao angau utarejesha matumaini ya kusalia ndani ya Ligi Kuu msimu ujao.
“Licha ya timu yetu yetu kukaa katika nafasi mbaya lakini hatutaingia kinyonge kwani tumeapa kuzindukia katika mchezo huu kwani ushindi utatuongezea morali zaidi ya kupambana katika mechi zetu zilizosalia ili kuweza kusalia ndani ya Ligi msimu ujao,” amesema Mjengwa.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania