Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Imeelezwa kuwa wazazi wengi wamekuwa wakiogopa kuwapeleka watoto wao wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupata matibabu kwa sababu mbalimbali ikiwemo imani potofu.
Huku moja ya chanzo cha watoto kuzaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi ikielezwa kuwa ni ukosefu wa elimu na imani potofu kwa jamii juu ya matumizi ya dawa za folic kwa wajawazito na wale wanaotaka kubeba mimba.

Hayo yamebainishwa Novemba 27,2025, kwenye warsha ya siku moja iliyokutanisha wataaamu wa afya kutoka wilaya nne za mkoa wa Mwanza,ikiwemo Ilemela, Nyamagana,Magu na Misungwi yaliondaliwa na Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA),kupitia mradi wa Wezesha mtoto unaofadhiliwa na Beyond Inclusive.
Mafunzo ya hayo kwa wataalam wa afya yamelenga kuwajengea uwezo wa kuwahudumia watoto wenye changamoto hiyo mara wanapofikishwa kwenye hospitali au vituo vyao vya afya.
Akizungumza katika warsha hiyo,Ofisa Mradi wa Wezesha mtoto kutoka MWADETA,Peter David,amesema wameamua kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya kutoka Wilaya hizo kwani kuna watoto wengi wenye changamoto hizo wanapotoke.
David amesema,wanaelewa kuna wazazi ambao wanaogopa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu, hivyo kupitia wataalam hao watakuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuwafichua.
“Tunatamani kuona pindi watoto wenye changamoto hiyo wanapobainika kwenye hizo wilaya iwe rahisi kupata huduma.Pia watoto wanaofichwa itakuwa rahisi kwa jamii kuwabaini kwakuwa huduma za matibabu zitakuwa zinapatikana kwenye vituo na hospitali za wilaya husika,” amesema David.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo,uti wa mgongo na mishipa ya fahamu,kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando,Misso Mpeji, ameeleza matatizo ya kichwa kikubwa na mgongo wazi huchangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa madini pamoja na tatizo la kiukuaji.
Dkt. Mpeji amesema sababu ya ugonjwa wa mgongo wazi hutokea wakati viungo vya binadamu vinavyotengenezwa hivyo mgogo kushindwa kufunga vizuri.
“Utafiti wa tatizo la mgongo wazi umebainisha kuwa upungufu wa madini ya folic huchangia tatizo hilo na wakati mwingine ni kutokuwepo kwa vimeng’enyo,” amesema Dkt.Mpeji.

Pia amesema,visababishi vingine vinavyochangia mtoto kuzaliwa na mgongo wazi ni pamoja na matumizi ya vilevi kwa wanawake wajawazito, matumizi ya dawa za degedege au kifafa pamoja na mimba ya watoto pacha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt.Jesca Lebba, amesisitiza mambo makuu manne ambayo ni pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii, kuimarisha mfumo wa rufaa na ushauri wa awali.
Huku akiwasisitiza wataalam hao kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili kuhudhuria kliniki mapema mara anapopata ujauzito jambo litakalosaidia kudhibiti tatizo la magonjwa hayo.



More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama