*Asisitiza ulinzi na usalama waimarishwa kuelekea uchaguzi mkuu
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limetoa wito kwa wananchi kutumia haki yao ya msingi kupiga kura na kufuata utaratibu kwa kurejea nyumbani baada ya zoezi hilo na siyo kubaki kwenye vituo,siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025.
Huku likisisitiza kuwa ulinzi na usalama umezidi kuimarishwa wakati wote na limejipanga kuimarisha zaidi siku ya uchaguzi mkuu na baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.
Akizungumzia na waandishi wa habari Oktoba 27,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,amesema,mwananchi hawezi kupiga kura kisha akabaki kwenye kituo na badala yake watumie hali yao kuchagua viongozi wanaowataka kisha wakaendelee na shughuli zao za kawaida.
“Hatutamani kuona makundi ambayo yanaweza kuchochea vurugu, kazi ya mwananchi ni kupiga kura na kuondoka.
Kila mtanzania anawajibu wa kulinda amani na jeshi la polisi halitavumilia vitendo vyovyote vya uvunjaji wa amani,”amesisitiza Mutafungwa.
Amesema,ulinzi na usalama umeimarishwa kuelekea siku ya kupiga kura na baada ya uchaguzi mkuu,ambapo doria na misako dhidi ya uhalifu na wahalifu inaendelea kwa nguvu zote na askari wa vikosi vyote wameongezwa katika mitaa mbalimbali ya Mkoa huo kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti uhalifu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza.
Pia kwa upande wa doria ndani ya Ziwa Victoria, askari wa kikosi cha wanamaji wameendelea kuimarisha doria ili kudhibiti uhalifu majini.Â
“Kwa upande wa usalama barabarani, tumeimarisha mifumo ya doria za masafa marefu kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya barabara hususani vyombo vya moto kwa madereva wanaofanya makosa hatarishi yanayoweza kusababisha ajali.Pia askari wetu wamepangwa kwa ajili ya kuongoza misafara ya viongozi mbalimbali wa kitaifa na wageni wanaoingia katika Mkoa wetu,” amesema Mutafungwa na kuongeza:
“Tunaomba wakazi wa Mkoa wa Mwanza na wageni kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za uhalifu, wahalifu na utii wa sheria bila kushurutishwa ili shughuli hiyo ifanyike kwa amani na utulivu na Mkoa uendelee kuwa salama hata baada ya uchaguzi kumalizika,”.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi