Na Daud Magesa, Timesmajira online, Mwanza
Akitoa ufafanuzi huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Wilbrod Mutafungwa katika taarifa yake amesema,jeshi hilo linapenda kutoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kumhusu Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijiji na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata Pamba kiitwacho Mwalujo Ginnery, kilichopo Kijiji cha Mwalujo, Wilaya ya Kwimba, Hamis Andrea Kigwangala, kudaiwa kumpiga risasi mlinzi wake Jumanne Omary Misango (66),katika mguu wa kulia.
Mutafungwa ameeleza kuwa tukio hilo linadaiwa kutokea Machi 22, mwaka huu, majira ya saa 11:00 jioni huko katika kiwanda cha kuchakata Pamba cha Mwalujo,kinachomilikiwa na Kigwangala, kilichopo katika Kijiji cha Mwalujo wilayani Kwimba.
Amesema taarifa ya awali zinaonyesha kulitokea wizi wa mali mbalimbali kiwandani hapo ikiwemo Gear Motor HP Radio made 02,Electrical Motor 05 na nyaya za umeme maarufu Armored Cable mita 25 vyote vikiwa na thamani ya 28,525,000(zaidi ya milioni 28).
Mutafungwa ameeleza kuwa Machi 22,mwaka huu,majira ya saa 11:00 jioni, Kigwangala alifika katika kiwanda hicho cha kuchakata pamba,kukatokea majibizano na kutolewana kati yake na mlinzi wake (Misango).
Siku hiyo hiyo mlinzi huyo alitoa taarifa kituo cha polisi Kwimba kuwa ameshambuliwa na kupigwa risasi kwenye mguu wa kulia na Kigwangala,ambapo baada ya taarifa hiyo polisi walikwenda kwenye kiwanda hicho kufanya ukaguzi lakini hakukuwa na viashiria vyovyote vya matumizi ya silaha ya moto.
Aidha mlinzi huyo alipewa PF3 (fomu namba tatu ya polisi) kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa uchunguzi wa kitabibu ambapo Dkt. Hamisi Kigwangala alihojiwa na kufunguliwa kesi ya shambulio na yuko nje kwa dhamana
.Kwa mujibu wa Mutafungwa uchunguzi wa awali umebaini hakuna jeraha wala mvunjiko wowote wa mfupa katika mwili wa Misango, kufuatia uchunguzi huo mlinzi huyo amefunguliwa jalada la uchunguzi (IR) kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa Ofisa wa Polisi na kuzua taharuki kwa jamii kuwa amepigwa risasi.
Kamanda huyo wa polisi amesema upelelezi wa kesi hizo mbili unaendelea, utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani,pia upelelezi wa wa tukio la wizi wa mali katika kiwanda hicho ulioripotiwa polisi Kwimba unaendelea.
Pia jeshi la polisi linatoa rai kwa wananchi kutojichukulia sheria mkononi,watumie njia sahihi kutatua migogoro inayowakabili wakishirikisha vyombo vya dola au taasisi zenye mamlaka, pia waendelee kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu zifanyiwe kazi haraka.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa