December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MUST yabuni mtambo wa kuchakata mafuta ya dizeli yanayotakana na chupa za plastiki

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

CHUO Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimebuni mtambo wa kuchakata mafuta ya dizeli yanayotokana na chupa za plastiki.

Akizungumza alipotembelea banda la chuo hicho katika amonyesho ya wakulima Nane Nane katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya,Makamu Mkuu  wa chuo hicho  Aloys Mvuma amesema,chuo hicho kimekuwa kikiibua wabunifu ambao hutengeneza teknolojia zinazotatua changamoto mbalimbali katika jamii ambalo ndilo lengo la ubunifu.

Amesema,katika maonyesho ya wakulima Nane Nane 2023 wamekuja kuonyesha teknolojia mbalimbali walizobuni wanafunzi kwa kushirikiana  na wanataaluma katika chuo hicho ikiwemo teknolojia ya kuchakata chupa za plastiki na kupata mafuta ya dizeli.

“Katika maonyesho ya Nane Nane hapa katika viwanja vya John Mwakangae tumekuja na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa ambazo zinatatua changamoto mbalimbali kwenye jamii ,kama vile kwenye kilimo,ufugaji,matumizi ya teknolojia kama akili bandia ‘artificial intelligence’,

“Lakini kimsingi kuna teknolojia kubwa ambayo mwanafunzi aliibuni na chuo kikamsaidia kuifikisha katika hatua ya kuchakata chupa za plastiki ambazo zimeshatumika kwenda kutengeneza mafuta ya dizeli kwa ajili ya kuendesha mitambo mbalimbali .”

Amesema,mtambo huo umefikia katika hatua nzuri na lengo kuu ni kuweka mazingira katika hali ya usafi badala ya chupa hizo kuendelea kuzagaa na kusababisha uchafuzi wa mazingira.

“Taka zile tunazichakata na kuwa mafuta ya dizeli ,mtambo huo sasa unaweza kutoa sample za mafuta za kutosha ambapo kwa kila kilo moja za chupa taka zinatoa lita moja ya mafuta,sasa ili mashine ifikie hatua ya kutoa mafuta ya kutosha inabidi kuwe na wadau mbalimbali wa kushirikiana na sisi kuweka rasilimali fedha ili kupata mtambo mkubwa zaidi wa kutoa mafuta mengi zaidi na kuleta manufaa kwa jamii na Taifa.”amesisitiza

Aidha ameiomba Serikali iendelee kuwekeza katika vijana ambao wamekuwa wakitoa mawazo ya ubunifu ambapo bunifu hizo zinaenda kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Kwa upande mwanafunzi wa chuo hicho aliyebuni mtambo huo Justine Bahati amesema mtambo huo una uwezo wa kuchakata takataka za plastiki na kuzibadilisha kuwa mafuta.

“Kama tunavyojua mazingira na kilimo ni vitu vinavyoenda sambamba kwa hiyo kupitia teknolojia hii itasaidia kutunza mazingiralakini pia kuimarisha kilimo kwa kuleta hamasa kwa wakulima kutumia mitambo kama vile matrekta na pampu za maji ili kuongeza tija kwenye kilimo .”amesema Bahati

Amesema taka za plastiki kilo moja zinaweza kutoa lita moja ya mafuta huku akisema mtambo huo unazalisha mafuta ambayo yatauzwa kwa bei ya chini hivyo itawasaidia waweze kumudu garama za uendeshaji wa mitambo ya kilimo .

“Mtambo huu unatoa mafuta aina dizeli na petrol lakini kwa hatua iliyopo sasa tunapata dizeli ,kwa hiyo tunahitaji kuifanyia ‘filtration’ili tuweze kupata petrol.”amesema Bahati

Amesema,mtambo huo ni umetengenezwa kupitia ufadhili wa Tume ya Sayansi na Teknlojia nchini (COSTECH) baada ya kushiriki mashindano ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2020 .

Amewashauri vijana kuchangamkia fursa ya ubunifu ili kujikwamua kiuchumi kwani kupitia bunifu hizo zinatengeneza ajira na kukuza uchumi.

Kwa mujibu wa Bahati mtambo huo umetumia kiasi cha shilingi milioni 25 kutengeneza mtambo huo ambazo ni pesa za ufadhili kutoka COSTECH huku akisema ili atengeneze mashine kubwa ya kuhudumia watu wengi zaidi inahitaji kiasi cha dola 50,000.