Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Kampala.
RAIS wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametoa wito kwa viongozi wa dini katika Nchi za Maziwa Makuu kuendelee kusisitiza umoja na amani katika mataifa yao, ili kufanikisha agenda ya maendeleo.
Amesema kuwa, maendeleo ya nchi za Maziwa Makuu hayawezi kuwa thabiti iwapo Wananchi hawatakuwa na amani wala umoja.
Huku akiwasisitiza kukemee suala la udini na ukabila unaoweza kuwagawa watu na kuhatarisha amani.
Rais Museveni ameyasema hayo Juni 3, 2024 wakati wa kilele cha siku ya kitaifa ya kumbukizi ya Mashashidi 22 wa Uganda iliyofanyika kanisa Katoliki Namugongo jijini Kampala nchini humo.
Pia Mke wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,Mama Maria Nyerere kutoka Tanzania,Mahujaji wa Kanisa Katoliki kutoka mataifa mbalimbali Afrika na duniani walihudhuria katika kilele cha siku hiyo pia walifanya hija ya maombi kwa siku kadhaa maeneo ambayo mashahidi hao 22 walifia lilipo jengwa Kanisa Katoliki Namugongo.
Taifa hilo huwakumbuka Mashahidi 22 wa Uganda kila mwaka waliouawa kwa mateso mbalimbali ikiwemo kuchomwa macho, kukatwa shingo mbele ya umati wa watu na Kabaka Mutesa wakaifia imani ya kanisa Katoliki na hatimaye kutangazwa watakatifu na kanisa hilo mwaka 1964 huku Serikali ya nchi hiyo kutangaza Juni 3 ya kila mwaka kuwa siku ya kuwakumbuka.
“Wakristo mdumishe amani, niwasihi viongozi wa dini zote nchi za Maziwa Makuu msinyamaze kusisitiza amani, umoja, upendo na mshikamano hapa Uganda kwa sasa udini tumepambana nao, huko nyuma umetusumbua sana,hatuwezi kupiga hatua kimaendeleo kama watu hawaishi kwa amani na wanamgawanyiko,”amesema Rais Museveni.
Ametolea mfano taifa la Tanzania lililoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa ni kinara wa amani na umoja kutokana na Mwalimu kuwaunganisha Watanzania.
“Mwalimu Nyerere alikemea vikali udini, ukabila na akafanikiwa, hutasikia mgawanyiko ama utengano kwa watanzania,”amesema Rais Museveni.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Uganda itaendelea kumuenzi na kuthamini kwa mchango wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutokana na kuisaidia nchi hiyo kupata uhuru na mataifa mengine barani Afrika.
“Mwalimu amesaidia sana ukombozi wa nchi za Africa, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Msumbiji hiyo ni kuonesha kwamba alisimamia maslahi mapana ya Waafrika na maendeleo yao,”amesema Museveni.
Juni Mosi, kila mwaka Taifa la Uganda huadhimisha siku ya Mwalimu Nyerere
ambapo kwa Tanzania huadhimishwa Oktoba 14 ya kila mwaka.
Ambapo mwaka huu pia limeadhimisha siku hiyo kwa kufanya misa ya kumuombea Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atangazwe mwenye heri pia atangazwe Mtakatifu.
Mgeni rasmi katika misa hiyo alikuwa Rais Yoweri Museveni ambaye aliwakilishwa na Waziri Mkuu wa Taifa hilo Robina Nabanja na misa hiyo ilifanyika katika Kanisa Katoliki la Namugongo lilipo Jijini Kampala pamoja Mama Maria Nyerere, Mama Tunu Pinda na Watanzania.
Hotuba ya Rais Museveni iliyosomwa na Waziri Mkuu Nabanja katika misa hiyo, ilimuelezea Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi bora, mcha Mungu na aliyejitoa kwa ajili ya Waafrika si taifa la Tanzania pekee.
Ambapo serikali ya Nchi hiyo itaendelea kushirikiana na familia ya. Hayati Mwalimu Nyerere na taifa la Tanzania.
Bhoke Nyerere akizungumza kwa niaba ya Mama Maria Nyerere,amesema familia hiyo inafarijika kuona Serikali ya Uganda inathamini na kumuenzi Mwalimu Nyerere kama ilivyo kwa taifa la Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Robinson Wangaso ni Mkazi wa Musoma ambaye ni miongoni mwa Watanzania waliokwenda nchini Uganda kwa ajili ya hija, amewaomba Watanzania kuendelea kupendana na kutenda matendo mema yenye kumpendeza Mungu na wanadamu pamoja na kutunza amani na umoja wa kitaifa uliopo nchini.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya