December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mulunga ashinda kwa kishindo Umeya Ilemela

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

ALIYEKUWA Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, Renatus Mulunga amefanikiwa kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine baada ya kushinda kwa kupata kura za ndio 27 sawa na asilimia 100.

Ambapo katika nafasi hiyo Mulunga alikuwa mgombea pekee huku kwa nafasi ya Unaibu Meya imechukuliwa na Manusura Sadick ambaye ni Diwani wa Kata Buzuruga kwa kupata kura zote 27 za ndiyo sawa na asilimia 100 ambapo pia katika nafasi hiyo mgombea alikuwa pekee yake.

Akizungumza baada ya kuapishwa katika hafla ya uapisho wa Madiwani wateule wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela uliofanyika Desemba 2 mwaka huu katika Halmashauri hiyo, Mstahiki Meya huyo amesema, ataendeleza ushirikiano kwa kila kata na wataenda kwa kasi zaidi katika kutatua changamoto za wananchi na kutelekeza ahadi walizozitoa wakati wa kuomba kura ili kufikia maendeleo wanayoyatarajia.

Kwa upande wake Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Manusura Sadick, ameomba ushirikiano ili kufanikisha yale walioyaahidi kuyatekeleza hivyo wanaenda kutelekeza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 katika kutatua matatizo ya wananchi na kuleta maendeleo huku akiahidi kulinda na kuhifadhi rasilimali zote zinazopatikana katika halmashauri hiyi na kila kata itanufaika na rasilimali hizo.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula, amesema mchakato wa uchaguzi umeisha hivyo wanachotarajia kwa jamii siku zote ni ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja ili kutelekeza kauli mbiu ya ‘Ilemela ni yetu tushirikiane kuijenga’.

Kwa pamoja yeye na Madiwani watasimamia nidhamu na maadili katika halmashauri hiyi kwa upande wao na watumiaji kwa kuhakikisha kunakuwa na nidhamu pamoja na kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi na kuyafanyia kazi.

Pia watasimamia kikamilifu uimarishaji wa mapato pamoja na mfumo wa ukusanyaji wa mapato kuwa ya kielotroniki, utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Rais, Mbunge na Madiwani hivyo wataendelea kuboresha miundombinu ya barabara, sekta ya Afya, elimu na maji.

Akizungumza kwa niaba ya Madiwani hao, Diwani wa Kata ya Nyakato, Jonathan Mkumba amesema, baada ya kula kiapo Madiwani hao wanaenda kufanya kazi yale walioahidi wananchi kwa kushirikiana na watendaji katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii hivyo aliwaomba wananchi ushirikiano ili kufanikisha adhima hiyo.

Baada ya zoezi la kuwaapisha madiwani kukamilika, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga alizindua kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambacho kilikuwa na agenda tisa ikiwemo kuchagua wenyeviti wa kamati mbalimbali.

Hata hivyo jumla ya Madiwani 27 wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Kati yao ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula, Madiwani wa kata 19 na 7 wa viti maalumu waliapishwa.